METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 21, 2018

DKT TIZEBA ATOA SIKU 4 WAKULIMA WA MKONGE MKOANI TANGA KULIPWA FEDHA ZAO

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akitoa maelekezo ya serikali wakati wa kikao cha pamoja na wadau wa Kilimo cha Mkonge cha mkataba (SISO) kabla ya mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin Shigela akizungumza jambo kabla ya kumaribisha mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba kuongoza mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018.
Viongozi mbalimbali Mkoani Tanga wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin Shigela wakiagana na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018.
Wadau wa zao la Mkonge wakichangia mada wakati wa mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018.

Na Mathias Canal-WK, Tanga

Wakulima wa Mkonge Mkoani Tanga wamempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba kupitia agizo lake alilolitoa kwa Kampuni ya Katani Limited kuhusu kulipa madeni ya wakulima ndani ya siku nne kuanzia 21 Juni 2018 hadi 26 Juni 2018 Kwa madeni ya muda mrefu ya wakulima wa zao hilo jambo lililopelekea kupunguza ufanisi na tija ya Kilimo Kwa wakulima hao.

Dkt Tizeba ametoa agizo hilo jana 21 Juni 2018 akiwa kwenye mkutano na wadau wa Kilimo cha Mkonge cha mkataba (SISO) unaotekelezwa kwenye mashamba matano ya Hale, Magunga, Magoma, Mwelya na Ngombezi yaliyo chini ya miliki ya Bodi ya Mkonge Tanzania. 

Katika Mkutano huu uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Martin Shigela sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe Godwin Gondwe, Msajili wa Hazina, Mtendaji wa BRELA, Muwakilishi wa mwanasheria Mkuu wa serikali, Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge na wataalamu wengine; Waziri wa Kilimo Mhe Tizeba ametoa agizo hilo Kwa Uongozi wa mfumo wa Kilimo cha wakulima wadogo wa kilimo cha Mkonge cha mkataba (SISO), Kampuni ya Katani ltd ambayo ndio mnunuzi pekee wa Mkonge wa mkulima na Bodi ya Mkonge Tanzania.

Sambamba na agizo hilo pia Mhe Waziri ameiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kupitia upya mikataba yote iliyopo Kwa kushirikisha Bodi yenyewe, Kampuni ya Katani na wadau wa zao hilo haraka iwezekanavyo ili kurekebisha makosa yaliyopo.

Aidha, ameitaka Bodi hiyo ya Mkonge Tanzania kuitisha kikao na wadau wote wa zao hilo ili kupitia upya utaratibu wa makato ya mgawanyo wa mapato katika kusindika zao la Mkonge.

Mhe Dkt Tizeba aliongeza kuwa hati za miliki ya mashamba zitapaswa kutolewa Kwa wahusika Mara baada ya kujiridhisha na mchakato utakapokamilika huku akiwataka wakulima kulipa malimbikizo ya kodi ya ardhi.

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba amemaliza ziara ya siku moja ya kikazi mkoani Tanga huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin Shigela Kwa umakini na uwajibikaji katika kusimamia sekta ya Kilimo hususani zao la Mkonge mkoani humo.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com