Mgeni rasmi-Waziri wa
kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa sherehe za ufunguzi wa
masoko ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima
Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018. Picha Zote Na Mathias Canal, WK
Waziri wa kilimo Mhe.
Dkt Charles Tizeba akimkabidhi cheti cha pongezi Mkulima Jonas Blakali kutoka
Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita ambaye ameshika nafasi ya tatu katika msimu wa
kilimo cha tumbaku wa mwaka 2017/2018 wakati wa sherehe za ufunguzi wa masoko
ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima
Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Mgeni rasmi-Waziri wa
kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akikata utepew kuashiria ufunguzi wa
masoko ya tumbaku Kitaifa katika sherehe iliyofanyika kwenye viwanja vya kata ya Mwendakulima
Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Waziri wa
kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akishuhudia ununuzi wa tumbaku wakati wa sherehe za ufunguzi wa
masoko ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima
Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Baadhi ya wakulima wa tumbaku wakishuhudia sherehe za uzinduzi wa ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Zainab Telack akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba wakati wa sherehe za ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Na
Mathias Canal, WK, Kahama-Shinyanga
Waziri wa kilimo Mhe
Dkt Charles Tizeba amefungua masoko ya tumbaku Kitaifa huku akitoa onyo kali
kwa wakulima waliolima zao hilo nje ya mfumo wa ushirika kwa mujibu wa sheria
ya zao hilo kwa kuwataka kuacha mara moja kwani serikali itashughulika na wote
wanaokiuka taratibu za kilimo hicho.
Dkt Tizeba ameyasema
hayo leo 12 Juni 2018 katika viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama
Mkoa wa Shinyanga wakati akihutubia mamia ya wakulima wa tumbaku kwenye sherehe
za ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa.
Dkt Tizeba amemuagiza
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Zainabu Telack kufanya kikao na Wakuu wa Wilaya
na Wakurugenzi wa Wilaya zote za Mkoa huo kuhakikisha wanazuia wananchi kulima
nje ya mfumo wa ushirika kwa mujibu ya sheria ya zao la tumbaku.
Alisema kuwa wigo wa
soko la tumbaku unazidi kuwa finyu kutokana na viongozi mbalimbali kuwakumbatia
baadhi ya wakulima wa tumbaku wanaolima nje ya mfumo wa zao hilo.
Katika sherehe hiyo Mhe
Dkt. Tizeba amekabidhi vyeti vya pongezi kwa wakulima waliofanya vizuri katika
msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 ambao ni mkulima Emmanuel Cherehani kutoka
Wilaya ya Ushetu aliyeshika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ni Jimson
Mwanjwenga kutoka Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya na Jonas Blakali kutoka Wilaya
ya Bukombe Mkoani Geita.
Awali akisoma risala
kwa niaba ya wakulima wa zao la tumbaku Tanzania Kaimu Meneja Mkuu TCJE Ndg Bakari
Kisia alisema kuwa zao la tumbaku limeanza kulimwa nchini Tanzania enzi za
ukoloni kwa kuanzia mikoa ya Ruvuma (Tumbaku ya Moshi) na Iringa (Tumbaku ya
mvuke) huku akisema kuwa umaarufu wa zao hilo umekuja mara baada ya masoko huria
kuanzishwa.
Kisia amepongeza juhudi
za serikali katika misimu miwili ya mwaka 2016/2017 na 2017/2018 kwa kutatua
suala la kupanda kwa bei ya pembejeo huku akizitaja changamoto katika zao la
tumbaku kuwa ni pamoja na kupungua kwa mahitaji ya tumbaku, Kushuka kwa bei ya
wastani ya tumbaku, pamoja na Ukubwa wa riba za mikopo.
Akisoma taarifa ya
maendeleo ya zao la tumbaku Tanzania Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya tumbaku
Tanzania Dkt Julius Ningu ameitaja mikoa inayolima tumbaku kwa wingi kuwa ni
pamoja na Shinyanga, Kagera, Geita, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya, Morogoro,
Iringa, Ruvuma na Mara huku akiutaja mkoa wa Tabora kuongoza kwa uzalishaji kwa
takribani asilimia 50 ya tumbaku yote inayozalishwa nchini.
Alisema kuwa zao la
tumbaku lina mchango mkubwa katika pato la Taifa ambapo pato la mkulima
limeongezeka kutoka shilingi za kitanzania 2,242,030 mwaka 2011/2012 hadi
shilingi 5,982,745 mwaka 2016/2017 ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia
166.8
Makusanyo ya ushuru wa
Halmashauri za Wilaya yameongezeka kutoka shilingi bilioni 10.8 mwaka 2011/2012
hadi shilingi bilioni 14.8 mwaka 2016/2017 ongezeko la asilimia 37. Huku mapato
ya fedha za kigeni yakiwa yameongezeka kutoka dola milioni 302.8 mwaka 2011
hadi dola milioni 343.9 mwaka 2016/2017 ongezeko la asilimia 14.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment