Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waangalie umuhimu wa kutumia mifumo ya ulinzi wa miji ya kieletroniki (City Surveillance System) ili kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 24, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na viongozi wa Jeshi la Polisi kwenye viwanja vya Mbweni, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam baada ya kuzindua vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni.
“Katika suala zima la kuimarisha usalama, napenda niwape changamoto Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi ili zitoe kipaumbele kwenye matumizi ya City Surveilance System (CCTV). Usimikaji wa mifumo hiyo utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao,” amesema.
Waziri Mkuu amesema tayari Jiji kama Nairobi la nchini Kenya linatumia mifumo ya aina hiyo na kwamba uwepo wa mifumo hiyo, na haoni ni kwa nini Tanzania bado haijawa na mifumo kama hiyo.
Amesema uwepo wa mifumo hiyo, utasaidia si tu kutambua kwa wepesi wahusika wa matukio ya uhalifu kama vile ukwapuaji, wizi wa magari na uharibifu wa mali, bali pia utaongeza shughuli za kibiashara na utalii.
"Tanzania hatujaanza kutumia mifumo hii lakini ifike mahali, tuanze kubadilika. Tafuteni wataalamu wenye ujuzi watufungie mifumo hii ili iwe rahisi kufuatilia matukio mbalimbali. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani fuatilia mifumo hii ili tuanze na majiji yetu na tuweze kufuatilia matukio ya kihalifu barabarani na mitaani", amesema Waziri Mkuu.
"Nitoe rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi wachukue hatua za haraka kurahisisha upatikanaji wa matumizi ya mifumo hiyo hususan katika majiji yetu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watu na mali zao," amesema.
Mapema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni alimshukuru Rais Dkt, John Pombe Magufuli kwa kukubali kutoa kiasi cha sh.bilioni 10 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za polisi.
Alisema kutokana na fedha hizo, nyumba takriban 400 za askari polisi, zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo hivyo vitatu, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro alisema ujenzi wa kituo cha Mburahati umegharimu sh. bilioni 1.2, Kiluvya (sh. milioni 227) na Mbweni (sh. milioni 667).
Alisema ujenzi wa vituo hivyo umeshirikisha wananchi wa maeneo husika, Jeshi la Polisi na wadau werevu ambao ni walipakodi wazuri na wazalendo zikiwemo taasisi na watu binafsi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MEI 24, 2018.
0 comments:
Post a Comment