WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dk.Hamisi Kigwangalla amekabidhi
magari kwa Halmashauri 6 kwa ajili ya kupambana na vita dhidi ya ujangili.
Magari hayo amewakabidhiwa Wabunge leo katika ofisi
za Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii Jijini Dodoma.
Wabunge waliokabidhiwa magari hayo ni wa Bunda
Vijijini,Boniface Getere ,Itilima,Njalu Silanga ,LongIdo,Dk.Steven
Kiruswa,Mbulu Vijijini Flatei Massay,Tanganyika,Moshi Kakoso huku Mbunge wa
Ngorongoro,William Ole Nasha yeye hakuweza kufika kutokana na kubanwa na
majukumu mengine.
Wabunge hao wamepokea kwa niaba ya Halmashauri hizo.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi magari hayo,Dk.Kigwangalla amesema
jumla ya Halmashauri 6 zinatarajiwa kunufaika na magari hayo.
“Tunakabidhi magari ambapo Halmashauri 6 zitanufaika ambayo
yanatokana na jitihada za Waheshimiwa Wabunge kutusumbua sana lakini pia utashi
wao katika kuunga mkono katika vita dhidi ya ujangili.
“Lakini pia magari haya yatatusaidia kwenye doria katika maeneo
hayo lakini pia ‘kurespond’ haraka kesi za wanyama
waharibifu mfano katika maeneo kama kule Bunda
Vijijini katika vijiji vya Mugumu na Mgeta kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana
wa wanyamapori na makazi ya watu.
“Lakini bahati mbaya Halmashauri zinakuwa hazina usafiri wa
‘Kurespond’ haraka kwenda kuwaondoa wale wanyama hivyo tumeona tuwape gari kama
kule kwa wahadzabe,Longido tumeona tuwape magari.
“Maeneo kama Itilima hata juzi nilishuhudia kwa
masikitiko makubwa watu wawili wakipoteza
maisha kwa kuvamiwa na
Tembo na Tembo hao walihamia kabisa wakaweka kambi na wamemaliza mazao ya
wananchi na wamesababisha vifo.
“Tuliona tuzisaidie Halmashauri zetu hivi ili na zenyewe zipate
vyombo vya uhakika ili waweze kufika haraka.
Waziri huyo amesema sambamba na makakati huo pia Serikali
inakusudia kujenga madungu kwa ajili ya kuangalia wanyama tokea
wakiwa mbali ndani ya hifadhi.
Pia amesema wanatarajia kuweka uzio wa mizinga ya
nyuki ili kuzuia wanyama kama Tembo wasitoke katika maeneo ya hifadhi.
“Wenzetu hawa wa Tanganyika wao wana msitu mzuri wa Tongwe ambao
una nyani na tayari tumeishapitisha msitu wa Tongwe uwe hifadhi na utakuwa
chini ya Halmashauri hivyo tumeona tuanze kuwajengea uwezo wa usafiri ili waweze
kuuendesha.
Dk Kigwangalla ametoa angalizo kwa halmashauri zilizopewa magari
kuwa yatumike kwa shughuli za maliasili pekee na sio zingine
“Napenda kutoa angalizo kwa hizi halmashauri zilizopewa haya
magari yatumike ipasavyo kuanzia ulinzi wa maliasili uendelezaji wa maliasili
na kutoa elimu kwa wananchi na zisitumike kwa shughuli zingine,”
“Naomba suala hili lizingatiwe na tayari tumeishamwelekeza
Katibu Mkuu ataandika barua mahususi ambayo itatoa maelekezo mahususi na kama
kutakuwa tofauti tunaweza kuchukua hatua ikiwemo kuyachukua magari
yetu,”alisema
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Maj. Gen. Gaudence
Milanzi amesema wametoa magari hayo kutokana na maelekezo ya Waziri wa Wizara
hiyo Dk.Kigwangalla kuwa yatolewe magari katika maeneo ambayo yanauhitaji wa
kulinda uhifadhi na wanyamapori.
“Waziri umeelekeza tutoe magari kwa baadhi ya maeneo ambayo ni
muhimu kwa ajili ya kulinda malisili zetu na leo tunawakabidhi hawa Waheshimiwa
Wabunge,”alisema
Naye Mbunge wa Mbulu Vijiji, Flatei Massay alimshukuru Waziri
kwa kuwapatia magari hayo huku akiahidi kuwa yataenda kutumika kwa mahitaji
yaliyokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment