Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu
Serikali imetoa jumla ya Vitabu 297,
891 kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi wa Darasa la kwanza mpaka darasa
la Tatu Mkoani Simiyu
Akizungumza kabla ya makabidhiano ya
vitabu hivyo Mjini Bariadi, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Ndabazi
Stephano amesema vitabu hivyo vitakidhi mahitaji ya wanafunzi kwa kuwa
idadi yake ni kubwa zaidi ya idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la
tatu ambao wako 261,257 kwa mkoa mzima.
Amesema azma ya Serikali ni
kuhakikisha kuwa kila shule ina vitabu vinavyojitosheleza na inaendelea
kuchapisha vitabu vya darasa la nne, ambapo Ofisi ya Rais TAMISEMI
imeanza kugawa vitabu hivyo katika mikoa mbalimbali na akabainisha kuwa mkoa wa
Simiyu nao utapewa vitabu hivyo.
"Tunaendelea kugawa vitabu vya
darasa la nne katika mikoa mbalimbali hapa nchini, hadi sasa vimegawanywa
katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara,
Ruvuma, Njombe, Iringa, Dodoma, Morogoro na awamu inayokuja ni Mikoa ya Kanda
ya Ziwa ukiwemo Simiyu” alisema Stephano.
“Vitabu hivi ni original (halisi) kabisa hamna kitabu feki hapa, maana
kuna taarifa zinasambaa mitandaoni kuwa vitabu hivi vimekosewa, niwaeleze walimu na wanafunzi mliopo hapa
vitabu hivi tunavyovigawa ni halisi na
havijakosewa” alisisitiza Ndabazi Stephano
Aidha, Bw. Gaitan Romwald kutoka
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) amesema vitabu hivi vinagawiwa kwa awamu, hivyo
vipo vitabu vingine vya darasa la kwanza mpaka la tatu ambavyo kwa Mkoa wa
Simiyu vitagawiwa pamoja na vitabu vya darasa la nne awamu ijayo.
Akizungumza na walimu na wanafunzi
walioshuhudia makabidhiano ya vitabu hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amewataka wanafunzi kuvitunza na kuvisoma ili viwasaidie katika
masomo yao, huku akiwataka walimu kuvitumia vitabu hivyo kuwafundisha
wanafunzi kwa moyo.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.
Julius Nestory ameishukuru Serikali kwa kuleta vitabu hivyo ambavyo amesema
vitatatua tatizo la upungufu wa vitabu uliokuwepo kutokana na ongezeko la
wanafunzi wanaoandikishwa mwaka hadi mwaka.
Walimu na wanafunzi pia wameishukuru
Serikali kwa kupeleka vitabu hivyo Mkoani Simiyu ambavyo vitakuwa chachu na njia mojawapo ya kuboresha mazingira ya
kufundishia na kujifunzia.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa
kuleta hivi vitabu, vitatusaidia katika masomo yetu maana tutajisomea ili
tujifunze na kupata uelewa zaidi" Eliasi John mwanafunzi Shule ya Msingi
Somanda A
“Kwa niaba ya walimu wenzangu na
wanafunzi wetu, napenda kuishukuru Serikali kutuletea vitabu hivi, vitakuwa
msaada mkubwa sana kwa wanafunzi wetu lakini hata kwetu pia na vitatusaidia
sana kuboresha mazingira yetu ya kufundishia watoto” Mwalimu Janeroza Gabriel
MWISHO
0 comments:
Post a Comment