Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amewataka
wafanyakazi mkoani humo kuchangamkia fursa
ya kutafuta viwanja katika maeneo ambayo uwekezaji mkubwa utafanyika ili waweze kujenga
nyumba na majengo mengine ya biashara ambayo yatawawezesha kujiongezea kipato
cha ziada.
Mtaka ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na wafanyakazi
wa Mkoa wa Simiyu katika Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi yaliyofanyika
kimkoa wilayani Itilima.
“Mwaka huu tutakuwa wenyeji wa NaneNane Kitaifa, karibu
na eneo la Nanenane tunatoa eneo kwa ajili ya kujenga Chuo cha Mipango
kajengeni hosteli wanafunzi wapange; tunajenga kiwanda cha vifaa Tiba Dutwa
jengeni nyumba watumishi wakapange, tunajenga VETA pale Bunamhala jengeni
vyumba vya biashara watu waje wapange Simiyu
mahali penye fursa nyingi” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka
amesema mkoa wa Simiyu ni Mkoa wenye agenda ya maendeleo hivyo akawataka wafanyakazi,
viongozi na wananchi kujiepusha kuwa watu wa matukio badala yake wajikite
katika agenda ya maendeleo ya Mkoa huo.
Awali akisoma
risala kwa niaba ya wafanyakazi Katibu wa Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa
Mkoa wa Simiyu(TALGWU) Wandiba Kongoro ameomba
Serikali izifanyie kazi changamoto mbalimbali za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na
madeni hususani ya uhamisho, likizo na matibabu, utararibu wa upandishaji wa
madaraja, baadhi ya waajiri kutoitisha mabaraza ya wafanyakazi na baadhi ya
waajiri kutowapa watumishi hodari zawadi zao.
Kongoro amesema
changamoto nyingine ni Michango ya wafanyakazi katika Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii kutolipwa kwa wakati hasakwa watumishi wanaolipwa kwa kutumia Makusanyo
ya ndani na akawaomba waajiri kulishughulikia hili katika kipindi hiki cha
mpito kabla mifuko haijaunganishwa ili kuepusha adha kwa watumishi
watakapostaafu.
Nao watumishi na
wananachi walikuwa na maoni mbalimbali kuhusu maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi Kimkoa ambayo yamefanyika kwa mara ya sita sasa tangu kuanzishwa
kwa Mkoa wa Simiyu mwaka 2012.
“Wana Itilima
tumeipokea Mei Mosi kwa furaha sana kama mnavyoona mwitikio wa wananchi na
wafanyakazi ni mkubwa, mpangilio wa matukio uko vizuri, nimevutiwa na utaratibu
wa kuwasoma wafanyakazi hodari mbele ya wenzao na kuwapa zawadi, hii itawafanya
wafanyakazi wengine kuwa na bidii ili nao wapate ” alisema Peter Karume Shimo
mwananchi kutoka Itilima.
“Siku hii
tumeipokea vizuri na Mkuu wetu wa Mkoa
ametuambia mambo mazuri ya kutufanya tuweze kujiimarisha kiuchumi kama watumishi
na vile vile kufanya kazi zetu kwa weledi, binafsi nawashauri wafanyakazi
wenzangu tufanye vile tunavyoelekezwa na viongozi wetu” alisema Mwamba Isaya
Venance Mwalimu wa Shule ya Msingi Munze wilayani Itilima,
Maadhimisho ya
siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi mwaka 2018 yamefanyika chini ya
Kaulimbiu inayosema “KUUNGANISHWA KWA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII,
KULENGE KUBORESHA MAFAO YA WAFANYAKAZI”
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment