METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, December 27, 2016

Agizo la Rais Magufuli kwa Serikali ya mkoa wa Singida laanza kufanyiwa kazi

Na Nathaniel Limu, Singida.
Serikali mkoani Singida, inatarajia kujenga kiwanja kikubwa cha ndege kitakachowezesha ndege kubwa za abiria na mizigo kutua, ikiwa ni maandalizi ya kunufaika na fursa lukuki za kiuchumi na kijamii zitakazopatikana,baada ya makao makuu ya nchi kuhamia jirani Dodoma.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Rehema Nchimbi wakati akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema wakati wo wote kuanzia sasa kazi ya kutafuta eneo la kujenga kiwanja hicho na taratibu zingine muhimu, zitaanza,na amewataka wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano.

“Msukumo wa ujenzi wa kiwanja kikubwa cha ndege,umekuja baada ya rais Dk.Magufuli kuutaka uongozi wa mkoa kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanja hicho. Ushauri au mapendekezo yanayotolewa na mkuu wananchi, hayo ni maagizo rasmi, kwa hiyo sisi tulio chini yake, tutajitahidi uwanja huo unajengwa haraka,” alisema na kuongeza.

“Maadamu Rais ameona umuhimu wa uwanja huo na yeye katika serikali yake,anao uwezo mzuri wa fedha,sisi wakazi wa mkoa wa Singida tunachopaswa kufanya,ni kuchangamkia haraka uwanja unapatikana na ujenzi unaanza.”

Akifafanua, alisema serikali ya awamu ya tano imelenga nchi kuwa kwenye uchumi wa kati, hivyo kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayochochea ukuaji wa uchumi, huwa haina kigugumizi katika kutoa fedha.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, mkuu huyo wa mkoa, alisema hatapenda kuona aina yo yote ya urasimu wa kuchelewesha ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege.

Kwa upande wa wananchi, amewataka watoe ushirikiano wa hali ya juu katika upatikanaji wa uwanja na ushirikiano huo usiishie hapo, uendelee hadi hapo kiwanja kitakapomalizika kujengwa.

“Mimi nitumie fursa hii kuwasihi wananchi katika hili la ujenzi wa uwanja wa ndege mkubwa, walipe kipaumbele cha kwanza na fidia wawe na subira. Waamini tu kwamba ni lazima watafidiwa. Nina uhakika kiwanja kitakapoanza kufanya kazi, wananchi watanufaika kiuchumi kwa kiwango kikubwa, na pengine watatanza kusema kiwanja hicho kimechelewa kujengwa,” alisema Dk. Nchimbi.

Katika hatua nyingi, alisema Serikali yake itafanya juhudi za kuhakikisha mkoa wa Singida, una kuwa wa viwanda vikubwa, ili kutoa nafasi makao makuu ya nchi Dodoma, kupumua na kujikita zaidi kwenye shughuli ya kuiongoza nchi.

“Pia nitahakikisha mkoa wangu unakuwa na uwezo wa kujilisha na kulisha makao makuu ya nchi. Tuna kila sababu ya kulifikia lengo hilo. Tutahimiza kilimo cha umwagiliaji na kuchimba mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo cha malisho ya mifugo,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com