Akizungumza wakati wa makabidhiano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataja wadau hao kuwa ni Ofisi yake iliyotoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuongezea posho ya walimu mahiri 40 wanaowafundisha wanafunzi hao pamoja na kununua mahitaji maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike.
Amesema wadau wengine ni Mbunge wa Itilima Mhe.Njalu Silanga aliyetoa kilo 500 za mchele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kilo 300, Mkurugenzi wa Itilima kilo 100 za mchele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi kilo 100 za mchele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi kilo 100 za mchele na Mkurugenzi Busega kilo 100 za mchele.
Aidha, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imeahidi kuchangia ng’ombe wawili na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu imeahidi kuchangia kilo 100 za mchele.
Mtaka amewashukuru wadau wote walioguswa kuwachangia wanafunzi hao wa kidato cha sita na akatoa wito kwa wazazi, viongozi na watu kutoka makundi mbalimbali kujitokeza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Idara ya Elimu katika kuwasaidia wanafunzi hao, ili waweze kujiandaa na kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa mwezi Mei.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa mwaka huu mkoa wetu unaingia kwenye mikoa itakayofanya vizuri zaidi Kitaifa, niendelee kuwaomba wanafunzi mliopo hapa mzingatie masomo siku 10 mtakazokaa hapa ziwe na manufaa kwenu na ninyi walimu 40 wafundisheni watoto kwa vipaji vyote mlivyojaliwa na Mwenyezi Mungu ili wafanye vizuri kwenye mtihani wao wa mwisho” alisema Mtaka.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya kambi hiyo ya kitaaluma kumalizika ndani ya hizo siku10 ufanyike mtihani ili kuwapima wanafunzi na akaahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni tano kwa walimu wataotunga maswali yatakayofanana na yale yatakayokuwepo katika Mtihani wa Taifa kwenye masomo yao.
Akizungumza kwa niaba ya walimu mahiri 40 wanaowafundisha wanafunzi kambini hapo Mwalimu Makame S. Makame kutoka Shule ya Sekondari Bariadi, amesema kwa namna walivyojitolea kuwafundisha wanafunzi hao wana imani kubwa kuwa mwaka 2018 utakuwa mwaka matokeo mazuri(Kidato cha Sita) ya kihistoria kwa Mkoa wa Simiyu.
Mwanafunzi Martina Simba kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na wadau wengine wote kwa misaada waliyoitoa na kusisitiza kuwa, kukaa kwao kambini hapo siku kumi hakutakuwa bure bali ni mwanzo mzuri wa safari yao ya mafanikio ya kuwafikisha katika mikoa itakayofanya vizuri zaidi katika Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2018.
Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita Mkoani Simiyu ilifunguliwa rasmi Aprili 3 ikiwa na jumla ya wanafunzi1003 kutoka shule 11 na walimu mahiri 40 kwa ajili ya kuwafundisha na inatarajiwa kufungwa Aprili 13, 2018.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment