METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 10, 2018

TASAF Yaendelea kuwanufaisha Wananchi Mkoani Simiyu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Awamu ya tatu umeendelea kunufaisha wananchi wakiwemo wakazi wa kijiji cha Nkoma wilaya ya Itilima na Nyakabindi wilaya ya Bariadi mkoaniSimiyu. 

Hayo yamebainishwa na baadhi ya Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini katika Kijiji cha Nkoma wilayani Itilima, Mtaa wa Nyakabindi na Mtaa wa Old Maswa wilayani Bariadi wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mmoja wa wanufaika wa Mpango huo, Bibi. Rebecca Masunga kutoka Mtaa wa Nyakabindi wilayani Bariadi, amesema TASAF imemsaidia kutoka katika umaskini sasa anapata kipato kinachomwezesha kujikimu, kwa kuwa amelima ekari tatu za pamba, ekari moja ya mahindi, ana ng’ombe 14 na mbuzi wanne na amenunua plau kwa ajili ya kulimia.  
“Nilikuwa maskini wa kutupwa , nilipoingia TASAF na kuanza kupokea zile elfu 36 nilikopa fedha nikalima nyanya ekari moja nikauza, nilipata shilingi laki sita nikanunua ng’ombe watatu wakakua;  baadaye nikawauza nikapata milioni moja na laki tano nilinunua ng’ombe 14 ndiyo hao mnaowaona tunawachunga sasa” alisema Rebecca Masunga
“Tuna kikundi chetu ambacho tunaweka fedha zetu baadaye tunagawana, tukisha gawana tunaenda kuzalisha, tunalima nyanya, kabeji, pamba halafu tunauza; mpango wangu wa baadaye niwe na mtaji mkubwa na nijenge nyumba bora ” alisisitiza Bibi.Masunga.
Nae Bibi. Stella Masamaki mkazi wa Old Maswa wilayani amesema kupitia mpango wa Kunusuru kaya maskini aliweza kukodi mashamba nakulima pamba, baada ya kuuza pamba akajenga nyumba bora ya vyumba vitatu na akatoka kwenye nyumba ya udongo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo amewapongeza wanufaika wa TASAF ambao wamezitumia fedha hizo kwa manufaa na akawashauri kuanzisha miradi midogo midogo na kuwatumia wataalamu wa kilimo pamoja na mifugo kuwasaidia katika uendelezaji wa miradi yao ya kilimo na mifugo.
Katika hatua nyingine Mratibu wa TASAF Wilaya  Itilima Bw. John Rajabu amesema wanufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini wameibua mradi wa maji ambao pia utawanufaisha na wananchi wengine, ambapo mpaka kukamilika kwake utatumia takribani milioni 15.
Wakati huo huo Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu wamefanya ziara katika Wilaya ya Meatu, Itilima na Maswa na kukagua miradi ya Maji, Afya na Elimu nakuwataka viongozi na watendaji katika maeneo husika kutimiza wajibu wao na kuhakikisha kuwa miradi yote inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma wanazostahili.
Sanjali na hilo wajumbe hao wamewataka viongozi kutambua fedha zinazochangwa na wananchi na kusimamia vizuri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,  ili zitumike kama ilivyokusudiwa.
MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com