METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 18, 2018

DC MTATURU AZINDUA TAWI JIPYA LA NMB HALMASHAURI YA ITIGI

KAIMU mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida Miraji Mtaturu amezindua tawi jipya la benki ya NMB Mitundu katika halmashauri ya Itigi huku akiipongeza benki hiyo kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Kutokana na kusogezwa kwa  huduma hiyo ya kibenki amewaasa wananchi  kutumia fursa ya uwepo wa tawi jirani na  shughuli zao za kiuchumi kama sehemu ya kujiletea maendeleo kwa kupata mikopo na kuweka pesa benki na sio mchagoni.

"Ndugu zangu NMB kwanza niwapongeze kwa hatua hii muhimu kwa maendeleo ya halmashauri yetu na wananchi kwa ujumla, hatua hii ni muhimu kwa kuwa ilikuwa inawachukua wananchi mwendo wa kilomita zipatazo 70 kufika Itigi mjini ili kuweza kupata huduma za kibenki jambo ambalo halikuwa zuri kiusalama,

"Mimi niwahakikishie kuwa kwa hatua yenu hii hamjakosea Mitundu ni mji unaokuwa haraka na una mzunguko mkubwa wa fedha kwani watu wake ni wafanya biashara na wakulima na wafugaji wazuri sana,hii ndio tafsiri ya NMB karibu yako wapo kila mahali,"aliongeza Mkuu huyo.

Mtaturu ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Ikungi amewataka wananchi kuwa waaminifu katika suala zima la mikopo itakayotolewa na benki hiyo ili wakuze biashara zao kwa kuhakikisha malengo ya mikopo hiyo yanakuwepo na hivyo kuwawezesha kurejesha fedha hizo kwa wakati.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi mkuu wa kitengo cha mteja mmoja mmoja na mauzo NMB makao makuu Omari Mtiga amemshukuru mkuu huyo kwa kukubali kuwazindulia tawi hilo na kueleza huduma mbalimbali zitakazopatikana ikiwemo akaunti ya nufaika ya wajasiliamali wadogo na akaunti ya watoto ambapo tawi hilo la Mitundu ni tawi la 216 yaliyopo nchi nzima.

Kwa upande wake Meneja wa NMB kanda ya kati Nsolo Mlozi ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ikiwemo ombi la mkuu wa wilaya la  kukiboresha kituo cha polisi cha  Mitundu.

"Mbali na uzinduzi huu tunatoa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya shilingi milion 5 vitakavyopelekwa kituo cha afya cha Mitundu na  mabati yenye thamani ya shilingi milioni 5 ili  kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule ya msingi Mitundu B,"alisema Mlozi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi  Ally Minja akizungumza katika uzinduzi huo amemweleza Mkuu wa Wilaya kuwa  Benki hiyo imekuwa ikitoa Sehemu ya faida zake kusaidia Huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo Elimu na Afya katika Halmashauri hiyo na kusema uwepo wa benki hiyo utasaidia kwenye ukusanyaji wa  mapato kwa kuwa  sasa watendaji na mawakala watakuwa hawaendi mwendo mrefu kufuata huduma ya kibenki.

Nae mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Manyoni Jumanne Makhanda na  Mbunge wa Manyoni Magharibi  Yahya Masare wamepongeza juhudi za serikali katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 .

"Sisi tunamuunga mkono mh Rais wetu dokta John Magufuli  kwa hatua mbalimbali za kimaendeleo anazochukua na nawapongeza wasaidizi wake wanaomsaidia huku wilayani wakiongozwa na mkuu wa wilaya yetu mh Mtaturu, anafanya kazi nzuri nzuri sana,"alisema mwenyekiti huyo.

Kijiji cha Mitundu kinazungukwa na kata zipatazo 5 na wilaya za jirani za mkoa wa Tabora ambazo ni  Sikonge,Uyui, na Chunya iliyopo mkoani Mbeya ambapo matarajio ya uzinduzi wa tawi hilo ambalo linafanya uwepo wa matawi  matatu kwa sasa katika wilaya ya Manyoni ni kuhudumia zaidi ya watu wapatao laki 3.

Mwisho.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com