Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewahakikisha Watanzania kuwa nchi bado iko salama na hakuna mgonwjwa yeyote mwenye ugonjwa wa Virusi vya Corona.
Dkt Ndugulile ametoa kauli hiyo akiwa Jijini arusha katika Ziara zake za kikazi ambapo waandishi wa habari walimuuliza juu ya tetesi za uwepo wa ugonjwa huo nchini, pamoja na kutaka kufahamu ukweli wa taarifa za mtu anayedai kuwa na dawa za ugonjwa huo.
“Niseme tuu kuwa Tanzania mpaka sasa hivi bado tuko salama na hakuna mgonjwa yeyoteambaye ameripotiwa na amethibitika kuwa na ugonjwa” amesema Dkt Ndugulile.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikifuatilia taarifa mbalimbali za washukiwa na watu wote ambao tunawahisi kuwa na ugonjwa huo na tumeweza kuwapima na kubaini kuwa hawana ugonjwa.
“Sambamba na hilo tumeendelea kuchukua tahadhari mbalimbali na mimi niko katika Mkoa huu wa Arusha na nitaenda Kilimanjaro kwenda kuangalia utayari” amesmea Dkt. Ndugulile na kuendelea kusema “ Nimepita hapa leo nimeongea na uongozi na nimeridhika na maandalizi ambayo tunayo
hapa katika Mkoa huu wa Arusha katika kudhibiti ugonjwa huo” Ameeleza Dkt. Ndugulile
Akijibu kuhusu mtu ambaye anasema kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa huo ambaye anajulikana kwa jina la Mosses Mollel maarufu kwa jina la “Nabii namba saba” aliyetoa taarifa za kuwa na dawa yenye uwezo wa kutibu virusi vya corona, Dkt Ndugulile amesema kuwa anazo taarifa za mtu huyo ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari akijitangaza kuwa anayodawa ya kutibu ugonjwa huo na kumtaka athibitishe kauli yake.
“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu anayejiita Nabii Saba kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa wa Corona ,ila hapa kwetu Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huyo ,tunachotaka huyo mtu atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa wa Corona” Amesema
Ndugulile Ameongeza kuwa iwapo atashindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua Kali za kisheria.
Amesema hadi sasa Serikali imetuma wataalamu wake kwenda kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali Vya kutoa huduma ya Tiba na kujitangaza kuwa anatoa Huduma ya kutibu ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa mataifa bado yanahaha kusaka Tiba ya ugonjwa huo.
Nabii Namba Saba ambaye ni mkazi wa Ngaramtoni Wilayani Arumeru,Mkoani Arusha amekuwa akijitangaza kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa huo wa virusi vya corona na kuweka mawasiliano yake kwenye mitandao.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa mtu yeyote anayetoa tiba asili na mbadala kwanza ni lazima asajiliwe na mamlaka husika ambayo ni Wizara ya Afya, pili lazima dawa zake ziwe zimesajiliwa na Wizara ya Afya na kusisitiza kuwa nabii huyo pia anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.
“Tuepuke kutoa kauli ambazo zinakwenda kuchanganya jamii, na endapo tutabaini mtu huyu hana sifa ambazo anasema kuwa nazo tutamchukulia hatua za kisheria” Amesema Dkt. Ndugulile.
0 comments:
Post a Comment