Asisitiza kwamba kazi ndiyo msingi wa maendeleo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wafanye kazi kwa bidii na maarifa kwa sababu kazi ndiyo msingi wa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Pia amewasihi wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipakani wahakikishe suala la kulinda mipaka hiyo linapewa kipaumbele ili kuimarisha amani na utulivu nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Machi 24, 2018) wakati akizungumza na wananchi alipowasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea.
Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema ili vijana waweze kupata maendeleo lazima wafanye kazi kwa bidii.
Pia Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipakani washirikiane na Serikali katika kuimarisha ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua ukarabati wa kituo cha afya cha Kata ya Mbekenyera na kuwaeleza wananchi dhamira ya Serikali ya kuwahudumia.
Amesema Serikali imetoa sh. milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya kujifungulia, maabara, wodi ya wanawake na wanaume na chumba cha upasuaji.
“Serikali imeamua kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao.”
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi hao waendelee kuiunga mkono Serikali yao, ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.
Pia, Waziri Mkuu amekabidhi gari la kubeba wagonjwa katika kituo hicho. Gari hilo limetolewa na Rais Dkt. John Magufuli ili kuimarisha huduma za afya kituoni hapo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, MACHI 24, 2018.
0 comments:
Post a Comment