Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (kushoto)
akiongozwa Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya anayestaafu
Bibi Mayasa Hashimu (Kulia) kuingia kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango kwa ajili
ya kufunga mkutano wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.
Afisa Elimu wa mkoa wa Pwani bwana Abdul Maulid
(kulia) aliyekaa mstari wa mbele akiwa pamoja na Maafisa wenzake wa Elimu wa
Mikoa na Wilaya wakimsikiliza mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI
Mhe.Joseph Kakunda (hayupo) pichani wakati wa ufungaji wa Mkutano wa Maafisa
Elimu wa Mikoa na Wilaya.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu
kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bibi Paulina Nkwama akizungumza kabla ya
kumkaribisha Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI kufunga Mkutano wa
Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Joseph
Kakunda akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na
Wilaya nchini.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Joseph Kakunda akimpongeza Bibi Dyness mosha ambaye ni mmoja wa Maafisa Elimu wanaostaafu mwaka huu.
...............................................................
Na Mathew Kwembe, TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema uamuzi wa Serikali kuwahamisha baadhi ya
Walimu wa shule za Sekondari wanaofundisha masomo ya sanaa kwenda kufundisha
shule za Msingi ulilenga kukabiliana na upungufu mkubwa wa walimu uliopo katika
shule za Msingi nchini na kamwe siyo adhabu.
Katika hotuba yake Waziri Jafo iliyosomwa
na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Joseph Kakunda
katika mkutano mkuu wa tano wa mwaka wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na
Wilaya Tanzania Bara jana mjini Dodoma,ametaka maafisa elimu hao kuwapanga
walimu kwa vigezo vilivyoweka na serikali na sio kama adhabu.
Amema kamwe
maafisa elimu wasiwapangie walimu hao wa sekondari kwenda shule ya msingi kwa
kigezo cha kutoa adhabu kwa walimu bali wazingatie vigezo hivyo.
Waziri huyo amesema
ameshaagiza kuwa kigezo cha mikondo ndio kiwe kigezo sahihi cha kupanga walimu.
“Nitalisimamia kwa karibu
sana suala hili, pia kigezo cha kupanga walimu shule za msingi kwa kutumia
idadi ya wanafunzi kinazinyima shule zenye wanafunzi wachache kuwa na walimu wa
kuweza kufundisha darasa la Awali hadi darasa la saba kwa ufanisi.
“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe.Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa
upo upungufu wa walimu kwa shule za msingi na walimu wa sayansi kwa shule za
sekondari,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo,
amesema kuna upungufu wa walimu wa shule
za msingi 85,000 nchini wakati ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule
za sekondari ni 21,000.
Waziri Jafo amesema kulingana na takwimu hizo serikali imeona
ni vema walimu hawa wa masomo ya sanaa wapelekwe kufundisha shule za msingi
kwani uamuzi huo wa serikali umezingatia suala la matumizi mazuri ya rasilimali
watu.
Amesema kutokana na wingi
wa walimu wa sanaa katika shule za sekondari mwalimu mmoja wa sanaa alikuwa
akifundisha chini ya vipindi 10 kulinganisha na mwalimu wa sekondari ambaye
alikuwa akifundisha vipindi 20.
Aidha Waziri Jafo pamoja na kutambua kuwepo kwa upungufu
mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo kwa upande wa
msingi na sekondari, ameziagiza halmashauri zote 185 kuweka nguvu katika
kukamilisha miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari pamoja na maabara.
Pia Waziri Jafo amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa
pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza agizo la
kununua magari na kutenga fedha za ununuzi wa magari kupitia bajeti za Mikoa na
Halmashauri.
Kuhusu wahitimu wa Darasa la saba wa mwaka 2018 kupata vyeti
vyao, Waziri Jafo amesema kuwa serikali imelichukua ombi hilo kwa uzito
unaostahili.
Katika risala yake, Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Umoja
wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya Bibi Mayasa Hashimu ameiomba serikali
iwasisitize wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya
ununuzi wa magari kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya.
Pia ameiomba serikali kuweka msisitizo wa pamoja katika
usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa Matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa,
maabara na hosteli shuleni.
0 comments:
Post a Comment