Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann(wa pili kushoto) na Anja Henke(kulia) mara baada ya kukamilika kwa semina kwa Viongozi, Maafisa na walimu wa Michezo mkoani humo (kushoto ) Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera.
Baadhi ya Wanafunzi wa kiume kutoka Shule ya Msingi Somanda A na Somanda B wakishiriki mbio za mita 400 katika Bonanza la Michezo lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani Simiyu wakimsikiliza Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann katika Semina iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka
Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo kuwasaidia Vijana wa Kitanzania
kutoka kwenye nadharia ya kufikiri kuwa michezo ni afya, urafiki na burudani tu ili waanze kufikiri michezo katika
mtazamo wa biashara na ajira.
Mtaka ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga semina
ya kuwajengea uwezo Maafisa Michezo,
Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni, kwa
lengo la kuchochea maendeleo ya Michezo
Mkoani Simiyu, ambayo yametolewa na Dkt. Angela Daalmann na Anja Henke ambao ni Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover
Nchini Ujerumani.
“Tumeleta
mafunzo haya tukiamini kuwa Maafisa Michezo wote ndani ya Mkoa wa Simiyu
watakuwa na msaada mkubwa kwenye kuwaandaa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye
nadharia ya kusema michezo ni afya, michezo ni upendo, michezo ni burudani ;
nataka Afisa Michezo akienda kwenye implementation(utekelezaji) vijana wa mkoa
wa Simiyu waanze kujenga vichwani mwao kuwa michezo ni ajira, michezo ni
biashara” alisema Mtaka.
“Katika Dunia ya
leo michezo ni biashara kubwa na ni ajira kubwa ya dunia ndiyo maana hapa
mmefundishwa kuhusu miradi, hili suala la michezo ni burudani, michezo ni afya, michezo ni urafiki na upendo libaki kama
jambo la pili” alisisitiza
Ameongeza kuwa
Maafisa Michezo pamoja na walimu wa michezo Mkoani Simiyu kupitia michezo ya
UMITASHUMTA na UMISETA wanapaswa
kuwatambua watoto/vijana wenye vipaji na kuwaandaa kibiashara ili wajue kuwa
vipaji vyao ni ajira zao za baadaye.
Aidha, amesema
Serikali mkoani humo imedhamiria kutangaza utalii na kukuza uchumi kupitia
sanaa, michezo na utamaduni na akabainisha kuwa Mkoa umeanza kutekeleza hilo
kupitia uanzishwaji wa Tamasha kubwa la
michezo na utamaduni maarufu kama “Simiyu Festival” ambalo linafanyika kila
mwaka na kwa mwaka 2018 litafanyika mapema mwezi Julai.
Naye Mtalaam wa Michezo kutoka
Jimbo la Hannover Dkt. Angela Daalmann amesema kwamba wamehamasika kutoa
mafunzo kwa maafisa, viongozi na walimu wa michezo mkoani Simiyu ikiwa ni mara
ya pili sasa, kutokana na utayari wa viongozi na watalaam mkoani humo katika
kuleta mapinduzi kwenye sekta ya michezo.
Afisa Michezo wa
Mkoa wa Simiyu, Bw.Emmanuel Athanas amesema mafunzo hayo yataamsha ari na
hamasa ya michezo kwa Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo na
kuwasaidia katika kuibua miradi mbalimbali itakayohusianishwa na michezo (sports
projects) sambamba na kuwatafuta wadau
mbalimbali kuwezesha miradi hiyo.
Naye Afisa
Michezo wilaya ya Meatu, Bw. Hassan Sengulo amesema mafunzo hayo yamewasaidia
kutambua namna sahihi ya kupata fedha kwa ajili ya uendeshaji wa michezo, hivyo watayatumia kuwaelimisha Walimu wa
Michezo na Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo namna ya kutatua changamoto ya ukosefu
wa fedha za kuendeshea michezo.
Semina hii
ilijumuisha jumla ya washiriki 27 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa
Simiyu na baadaye ikafuatiwa na Bonanza la michezo kwa wanafunzi wa baadhi ya
shule za msingi kushiriki mchezo wa riadha,
ambapo wanafunzi walipata nafasi ya kukimbia mbio za mita 100, mita 400
na mita 1500 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Somanda Mjini Bariadi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment