Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akimwagilia mti wa
mwembe alioupanda mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya
Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING
THEATER” wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Na Stella
Kalinga, Simiyu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia
Suluhu Hassan amewahimiza wananchi mkoani Simiyu kuchangia ujenzi wa
miundombinu ya elimu ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo ya
Sekta ya Elimu.
Mhe.Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Maswa Mkoani
Simiyu kwenye Mkutano wa hadhara
uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane wakati wa ziara yake mkoani humo.
Amesema Serikali
imeamua kutoa elimu bila malipo na kuwapunguzia wazazi mzigo wa kulipia gharama
za karo na michango mbalimbali ya uendeshaji wa shule lakini suala la kuchangia
ujenzi wa miundombinu ya elimu wananchi wanapaswa kuunga kuchangia ili kuunga
mkono juhudi hizo.
“ Tunapeleka
fedha katika shule zote za Msingi na Sekondari ili wanafunzi waweze kusoma
vizuri lakini kwenye suala la ujenzi wa matundu ya vyoo, madarasa, maabara
pamoja na kwamba Serikali ina wajibu wa kufanya hayo na ninyi wananchi mnao
wajibu wa kusaidia kufanya hayo” alisema Mhe. Makamu wa Rais.
Wakati huo huo
Mhe.Makamu wa Rais ameipongeza Wilaya ya Maswa kwa kuongeza ufaulu kutoka
asilimia 45 hadi asilimia 75 kwa mwaka 2017 na akakemea vikali tabia ya wanaume
wanaoua ndoto za watoto wa kike kwa kuwapa mimba , ambapo amesema jicho la
Serikali liko kwa watoto wa kike na itawachukulia hatua kali wote
watakaobainika kufanya hivyo.
Kwa upande wake
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe amesema watoto wa kike 28
wameripotiwa kuwa na mimba katika kipindi cha mwezi Desemba 2017 hadi sasa na
Serikali ya Wilaya kupitia Operesheni tokomeza Mimba imefanikiwa kuwakamata
watuhumiwa 15 na kati ya hao wawili wamehukumiwa miaka 30 jela kila mmoja.
Akizungumza kwa
niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri
wa Madini , Mhe.Stanslaus Nyogo amewashukuru viongozi wa Wilaya kuleta
mafanikio katika elimu ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu.
Katika hatua
nyingine Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu
Hassan mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya
ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER”
amewataka Watumishi wa Afya kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, amesema
Serikali itahakikisha inaboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
vituo vya Afya katika kila kata na kuboresha huduma za Afya ya Mama na Mtoto
ili kupunguza Vifo vya mama na mtoto.
Naye Naibu
Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Josephat Kandege amesema Serikali imekusudia
kujenga vituo vya Afya 286 kufikia
mwisho mwa mwaka 2017/2018 lengo
likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kupunguza mrundikano wa
wagonjwa katika Hospitali za Wilaya.
Mbunge wa Jimbo
la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki amesema pamoja na kuendelea kuboresha
sekta ya Afya kwa kujenga miundombinu, ni vema Serikali ikaajiri watumishi wa
Idara ya Afya kukabiliana na upungufu uliopo.
Mhe.Makamu wa
Rais amemaliza Ziara yake Wilayani Maswa ambapo amefungua Jengo la Upasuaji la
Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU
HASSAN OPERATING THEATER” na kuzungumza na wananchi katika Uwanja wa Nguzo
Nane.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment