METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, January 21, 2018

KITITA CHA TSH MIL 100 CHA KOPESHWA KWA WANAWAKE NA VIJANA MUFINDI

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William akikabidhi Mfano wa hundi kwa Afisa wa Benki, kama ishara ya kuruhusu utoaji Mikopo.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William, akikabidhi Hundi kwa mmoja kati ya Viongozi wa Vikundi 37.
Viongozi katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Vikundi wakiwa wameshika hundi zilizoambatishwa na Vocha.

Na Afisa Habari Mufindi    
                                                           
Jumla ya shilingi Milioni 100, zimetolewa kwa sharti la Mkopo kwa vikundi vya Wanawake na Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ikiwa ni utekelezaji wa takwa la sheria inayozitaka mamlaka za Serikali za mitaa  nchini kutenga asilimia 10 ya mapato  ya ndani kwa lengo la kuwakopesha vijana na Wanawake ili wajiajiri kupitia shughuli za kijasirimali hivyo kuboresha maisha yao.

Akisoma taarifa ya Mikopo hiyo, Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Hatibu Bwashehe, ametanabaisha kuwa, kati ya vikundi hivyo, vikundi 22 vya wanawake vimekopeshwa jumla ya shilingi Milioni 62, wakati vikundi 15 vya Vijana vimenufaika na Mkopo huo kwa kupata shilingi Milioni 38.

Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi kwa walengwa, mgeni wa heshima katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mh. Jamhuri William, amevitaka vikundi hivyo vielewe kuwa, fedha wanazopokea ni Mkopo hivyo, zitumike kulingana na maandiko waliyowasilisha badala ya kuzitumia kwa malengo tofauti kama vile kuchangia harusi au kununua mavazi ya kifahari na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa kutorejesha fedha za Serikali.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mh. Festo Ngina, amepongeza mwenendo mzuri ya urejeshaji Mikopo kwa vikundi vilivyokopeshwa kiasi cha shilingi Milioni 300 kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2016 – 2017 na akaongeza kuwa ili  hali ya urejeshaji izidi kuwa bora zaidi, Watendaji wa kata na Vijiji watahusika kufuatilia marejesho hayo kama ambavyo wanahusishwa  kwenye chakato kusajili vikundi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtendaji wa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Profesa Riziki Shemdoe, amewahimiza Vijana na Wanawake wa Halmashauri hiyo kuendelea kuwasilisha maombi kwa kuwa Halmashauri yake tayari imetenga fedha nyingine kiasi cha shilingi Milioni 140 ambazo watazikopesha baadaye mwezi ujao mara baada ya kukamilisha uchambuzi wa maandiko ambayo yatakuwa yanalenga kuanzisha viwanda Vidogo.

Aidha, wanufaika wa Mkopo huo ambao ni Wanawake na Vijana, wameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, kwa kuwathamini na kuwapatia mikopo hiyo huku wakiahidi kuzitumia kwa malengo na kurejesha kwa wakati.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com