METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 24, 2018

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAIPONGEZA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO KWA KUJENGA MAKUMBUSHO YA OLDUVAI GORGE


Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii  imeipongeza   Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  kwa kazi nzuri iliyofanya  ya ujenzi wa jengo la  makumbusho ya kisasa  katika Bonde la  Olduvai ya Gorge ambako ni chimbuko la historia ya  Binadamu.
Kamati hiyo imesema imeridhishwa na ujenzi wa jengo hilo ambalo litawavutia watalii na wanasayansi  wabobezi wa masuala ya Malikale kutembelea Makumbusho hiyo.
Kamati hiyo ilibainisha kuwa   Makumbusho hiyo mbali ya   kutumika kuingiza pesa kupitia watalii pia  inatumika  kama kielelezo na utambulisho muhimu wa taifa  katika kutangaza utamaduni wa Mtanzania ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa jana na Kamati hiyo  wakati ilipofanya  ziara ya kutembelea Ngorongoro Crater na  Makumbusho ya Olduvai Gorge  katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
 Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Kemilembe Luota ameipongeza Serikali pamoja na wataalamu kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuhakikisha kuwa  eneo la Olduvai Gorge linakuwa kivutio bora kwa ajili ya historia ya nchi na kivutio kikubwa cha Utalii duniani.
 ‘’ Sisi kama  Kamati tunaipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yote tuliyoyatoa  kwa  mara ya kwanza tulipokuja kwa vile tumeona kazi nzuri imefanyika.’’
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kutembelea makumbusho hiyo  kwa vile idadi ya watalii wa ndani aliyokutana nayo sio ya  kuridhisha.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema makumbusho hiyo inatoa ushahidi dhahiri kuwa hata  wazungu, mababu zao walitoka Afrika.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtama,  Nape Nnauye amesema Makumbusho hiyo hadi hapo ilipofikia imeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu hata hivyo ameitaka Wizara ihakikishe inaitangaza ipasavyo ili watalii wengi zaidi wazidi  kutembelea.
 Awali, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, FredyManongi  amesema tangu kuzinduliwa kwa makumbusho hiyo kwa wiki moja  imekuwa ikipokea zaidi ya  watalii wapatao 40000 hali inayopekelea   kuwa ni miongoni mwa Makumbusho inayofanya vizuri zaidi barani Afrika
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com