METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, December 11, 2017

Zaidi ya Wanafunzi Elfu 50 wafaulu Mtihani wao wa Darasa la Saba Mwanza

Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Michael Ligola akizungumza kwenye Kikao cha Uchaguzi wa  Wanafunzi mkoani hapa, wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2018 kilichofanyika katika ukumbi wa mkoa.
Judith Ferdinand, Mwanza
Wanafunzi  54,367 mkoani Mwanza wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (darasa la saba) mwaka 2017 na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018.
Wanafunzi hao ni kati ya watahiniwa 70,368 waliofanya mtihani wa kihitimu elimu ya msingi mkoani hapa, huku 33,976 wakiwa wasichana na wavulana 36,392 sawa na asilimia 99.3.
Hayo yalibainishwa jana  na Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola kwenye kikao cha uchaguzi wa  wanafunzi mkoani hapa, wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2018 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Ligola alisema wanafunzi 54,367 sawa na asilimia 77.3 mkoani hapa wamefaulu na kuchaguliwa  kujiunga na kidato cha kwanza huku kati yao wasichana wakiwa 26,393 na wavulana 27,974.
Alisema mkoa wa Mwanza umeshika nafasi ya nane  kitaifa, huku Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa, ikifuatiwa na Ilemela ambayo imeshika nafasi ya pili na ya tatu ikishikwa na Buchosa, ya nne ikienda kwa Sengerema, huku ya tano  ikishikwa na Misungwi, na ya sita ikienda kwa Kwimba na ya saba Magu wakati nafasi ya nane na ya mwisho ikishikwa na Ukerewe.
Aidha alizitaja shule zilizofanya vizuri katika mkoa wa Mwanza kuwa ni pamoja na Alliance ambayo imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya na mkoa na  tatu kitaifa, Mugini ambayo imekuwa ya kwanza kiwilaya, ya pili kimkoa na 13 kitaifa, Tulele English Medium kiwilaya ya pili, mkoa ya tano, kitaifa 31 huku Lake View ikishika nafasi ya tatu kiwilaya, ya sita kimkoa na 45 kitaifa.
Pia alisema jumla ya wanafunzi 204 wamepatiwa nafasi katika shule za bweni ambazo ni za vipaji maalumu na ufundi huku kati yao 70  ni  wanafunzi walio na mahitaji maalumu (walemavu) ambapo 44 wavulana na wasichana 26.
Kadhalika alisema kuna baadhi ya wanafunzi walishindwa kufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo magonjwa, kuhama, utoro na suala la mimba ambapo wilaya ya Ukerewe imeongoza kuwa na wanafunzi tisa wenye mimba,ikifuatiwa na  Magu ambao wapo wanane, hivyo lengo ni  kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kufanya mtihani sababu ya mimba.
Vilevile alisema,  kuna baadhi ya dosari zilijitokeza wakati wa mtihani huo kwa mwanafunzi wa  shule ya Alliance, Charles Mabula  ambaye  alifanya udanganyifu kwa kukutwa na majibu ya mtihani wa somo la hisabati kwenye mkanda wake hivyo baraza la mtihani limemfutia matokeo.
Hata hivyo alizitaka halmashauri ambazo hazijakamilisha madarasa wajitahidi kufikia januari wawewamekamilisha ili wanafunzi waweze kuanza masomo.
BMG Habari, Pamoja Daima!
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com