METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, December 5, 2017

TARURA WATAKIWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA BARABARA KWA WELEDI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA) Mkoani humo kusimamia utekelezaji wa Miradi ya  ujenzi wa barabara na madaraja kwa kuzingatia weledi.

Mtaka ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo, kichofanyika leo Mjini Bariadi  Mkoani humo.

" Nawaomba TARURA mfanye kazi kwa kuzingatia weledi, siyo madaraja yanajengwa mnapeleka karavati zinavunjika kabla daraja halijajengwa, mahali pa kuweka kokoto mnaweka udongo, mtaidhalilisha taaluma; ningeomba mzingatie weledi kwa sababu mkifanya vibaya wananchi watatushtaki watasema tumeanzisha wakala ambaye hana maana kwao" amesema Mtaka.

Ameongeza kuwa Uongozi wa Mkoa wa Simiyu haujapata shida juu ya miradi ya barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), hivyo ipo haja pia kwa TARURA kusimamia utekelezaji wa miradi yake katika ubora,  kwa kuwa Miradi hiyo imeondolewa katika Halmashauri (Mabaraza ya Madiwani) na kupelekwa TARURA, ili ipangiwe mipango  na kusimamiwa na wataalam pekee kwa lengo la kuonesha utofauti kiutendaji  na umuhimu wa Wakala huo katika kuwapa huduma bora wananchi.

Wakati huo huo Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi Bilioni 86.1 kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara ya Bariadi -Maswa yenye urefu wa Kilomita 49.7 kwa kiwango cha lami, ambayo amesema ikikamilika itaifanya Bariadi na Maeneo mengine ya Mkoa huo kama Malampaka(Maswa) kuwa  maeneo ya kibiashara.

Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri ya Wilaya Maswa kutumia fursa hiyo kujenga vituo vya mabasi vya kimkakati vitakavyoendana na kasi ya uingiaji wa magari mengi baada ya kukamilika kwa barabara ya Maswa-Bariadi na Ujenzi wa Reli ya “Standard Gauge” na  Bandari kavu itakayojengwa Malampaka wilayani Maswa.

Akiwasilisha taarifa ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Albert Kent  amesema Barabara ya Bariadi-Maswa itajengwa kwa kutumia fedha za Serikali ya Tanzania na itachukua muda wa miezi 24 mpaka kukamilika kwake, ambapo amebainisha kuwa Mkandarasi Kampuni ya M/s CHICO ameshawasili eneo la kazi(site).

Kwa upande wake  Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini ameomba wazo la marekebisho ya Viwango vya fedha zinazotakiwa kwenda TANROADS na TARURA ambalo lilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, lifanyiwe kazi ili TARURA wapate fedha na kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusaidia barabara za Halmashauri zisife.

Sagini ameongeza kuwa Halmashauri zishirikiane na TARURA kutafuta namna ya kuzifanyia matengenezo barabara za Vijiji ambazo haziko chini ya usimamizi wa wakala huo (TARURA), lakini  ni za muhimu kwa maendeleo ya wananchi hususani zinazounganisha vijiji ili kurahisisha mawasiliano kati ya kijiji na kijiji.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu,Mhandisi Peter Mosha amesema mwaka 2017/2018 Mkoa huo umeidhinishiwa zaidi ya shilingi bilioni sita kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 1780.87 , madaraja na makaravati katika Halmashauri zote sita za Mkoa kulingana na mahitaji na mpango wa bajeti wa Halmashauri husika.

Naye Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Wakala wa Barabara (TANROADS) unapaswa kuhakikisha barabara zote zinawekewa  vivuko ili kuwasaidia wananchi kuvuka kwa usalama.


Akipongeza kazi inayofanywa na TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga ameomba TANROADS kuona namna ya kufanyia kazi kona nyingi zilizopo katika barabara ya Bariadi-Lagangabili-Kisesa  pamoja na kuangalia upanuzi wa barabara mbalimbali zinazosimamiwa na Wakala huo ili zisisababishe uharibifu wa magari.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa huo(hawapo pichani) katika Kikao cha bodi hiyo kilichofanyika jana Mjini Bariadi, (kushoto) Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Jumanne Sagini na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,Mhe.Festo Kiswaga(kulia)
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijiji na Vijijini(TARURA) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Peter Mosha akiwasilisha taarifa ya wakala huo(Mkoa) kwa Wajumbe wa Bodi ya Barabara katikakikao cha bodi hiyo kilichofanyika Mjini Bariadi.
Meneja wa Wakala wa Barabara  (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Albert Kent akiwasilisha taarifa ya miradi inayosimamiwa na wakala huo Mkoani humo, katika Kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe.Dkt. Seif Shekalaghe akichangia hoja katika Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki akichangia hoja katika Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu kilichofanyika leo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika Kikao Bodi hiyo kilichofanyika leo Mjini Bariadi
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com