Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
SERIKALI kupitia
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) imesema ipo
mbioni kutoa mwongozo wa kuratibu na kusimamia viwango vinavyowiana
vinavyotarajiwa kutumika katika Vituo vyote
vya Upataji nafuu kwa watumiaji wa dawa za kulevya nchini.
Hayo yamesemwa jana Jijini
Dar es Salaam na Mratibu wa Mashirika yasiyo ya Serikali NGO’s kutoka (DCEA),
Salome Mbonile wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka minne ya kituo cha
upataji nafuu kwa watumiaji wa dawa za kulevya (PEDDEREF) kilichopo Kigamboni
Jijini Dar es Salaam.
Mbonile alisema katika
kuhakikisha kuwa mwongozo huo unaleta tija iliyokusudiwa, Serikali inatarajia
kuwashirikisha wadau wote katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya ili
waweze kutoa mapendekezo, ushauri na maoni ili kuweza kuisaidia jamii hususani
makundi ya vijana katika kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya.
"Kumekuwa na uwoga
kwa wananjamii kutembelea Sober House (Nyumba za upataji nafuu kwa watumiaji wa
madawa ya kulevya, lakini kupitia mwongozo huu tunataka kuweza viwango
vinavyofanana ili kutoa fursa kwa watu wote kutembelea makazi haya"
alisema Mbonile.
Mbonile alisema
mapambano ya vita dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya nchini hayana budi
kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo na hivyo Serikali itaendelea
kutoa ushirikiano wa na asasi, taasisi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa jamii ya
Kitanzania hususani vijana inaendelea kuwa salama na kuondokana na matumizi ya
dawa za kuelvya.
Aliongeza kuwa hadi
sasa Tanzania ina jumla ya Nyumba za upataji nafuu kwa watumiaji wa dawa za
kulevya 25 pamoja na Asasi 16 zinazotoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua
madhara mbalimbali yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo hatari ya
maambuzi ya magonjwa mbalimbali pamoja na vifo.
Aidha aliongeza kuwa
Serikali itaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii yenye
malengo ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya nchini, hatua inayolenga
kuwaunga mkono na kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa kadri
inavyowezekana.
“Nyumba za upataji
nafuu kwa watumiaji wa dawa za kulevya nyingi zinajengwa na waliowahi kutumia
dawa za kulevya na Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za mashirika haya na
kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuviweza kutekeleza vyema majukumu yake”
alisema Mbonile.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa PEDDEREF, Nuru Ahmed alisema suala la matumizi ya dawa za kulevya
limekuwa kubwa hususani kwa makundi ya vijana na kuwataka wazazi kushikamana
kwa pamoja badala ya kutupiana lawama pindi mtoto anapoanza kujihusisha na
matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema kuwa ujenzi wa
malezi mapya ya vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya, yanawezeakana
iwapo wadau wote hususani jamii zitajihusisha katika kukemea unyanyapaa ambao
umekushika kazi katika jamii, hatua inayochangia kufifisha jitihada
zinazofanywa na Serikali na mashirika mbalimbali nchini.
“Kituo chetu kina jumla
ya walaibu 58 wakiwemo wanawake 16 na wanaume 42, tunashukuru kwa ushirikiano
tunaoupata kutoka kwa Serikali na kuwaomba wadau wengine waendelee kushirikiana
katika kujenga jamii salama kwa mustakabali wa kizazi chetu” alisema Nuru.
Naye Mraibu aliyepata
nafuu katika utumiaji wa dawa za kuelvya, Amina Mbonde alisema alitumia nusu ya
uhai wa maisha yake katika kupambana kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, na
kukipongeza kituo cha PEDDEREF kutokana na mwamko wake wa kuwaweka pamoja
walaibu wa madawa ya kulevya na kuwaonyesha mwanga mapya wa maisha yao.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment