WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na utoaji
wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka
mikanganyiko Serikalini.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne,
Novemba 7, 2017) wakati akifungua Kikao Kazi cha Baraza la Mawaziri
kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema ni
vema viongozi hao kabla ya kutoa matamko
wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama
lipo katika bajeti za wizara zao.
Pia amewataka viongozi hao
wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa
Rais Dkt. John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.
“Tunao wajibu mkubwa
kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili
kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na wananchi wote kwa
ujumla.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka
viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za Wabunge na
kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
Pia amewataka wafanye
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo
inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya
Serikali.
Waziri Mkuu amesema Mawaziri na Naibu Mawaziri wanatakiwa
wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017
hadi 2020/2021.
Pia wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt. Magufuli
wakati wa kampeni za uchaguzi. (mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU, S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO,
NOVEMBA 08, 2017.
0 comments:
Post a Comment