Jimbo la Ilemela limepokea ugeni wa wataalamu wa masuala ya Tehama na Ardhi kutoka nchi ya Korea ya kusini kwa lengo la kusaidia uboreshaji wa makazi na ardhi ndani ya jimbo hilo kwa kutumia teknolojia ya kisasa
Akizungumza mara baada ya kuwasili jimboni humo kiongozi wa msafara wa Ugeni huo ndugu Lee, Kwang Se amesema kuwa safari yao ndani ya Jimbo la Ilemela itajikita katika kubadilishana utaalamu juu ya masuala ya ardhi kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayohusisha utumiaji wa ndege ndogo maarufu kama DRONES hasa katika masuala ya upimaji, ramani na mipango miji kutaposaidia kuzuia ujenzi wa makazi holela, udhibiti wa mapato ya serikali kupitia kodi za ardhi na kusaidia upangaji wa mji
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa huu ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Jimbo lake kupitia mashirikiano aliyoyaanzisha baina ya Jimbo lake na nchi ya Korea kusini huku akiwaasa wananchi wa Jimbo la Ilemela kutumia vizuri fursa zinazojitokeza kutokana na mahusiano baina ya pande hizo mbili katika kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wao
‘.. Huu ni muendelezo wa jitihada tulizoanza kuzifanya pale mwanzo za kuhakikisha tunatekeleza miradi mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Ilemela kupitia ushirikiano tuliouanzisha na wenzetu wa nchi ya Korea, Niwaombe wananchi na viongozi kutoa ushirikiano ili tuweze kujiletea maendeleo sambamba na kutumia fursa zote zitakazojitokeza kupitia mahusano haya …’
Aidha ugeni huo kabla ya kuanza utekelezaji wa shughuli zake wilayani Ilemela kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi kutoka Wizara ya ardhi, Ofisi ya ardhi Kanda ya Ziwa na wataalamu wa ardhi kutoka Manispaa ya Ilemela asubuhi ya leo ulifanikiwa kuzuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Mhe John Mongela na kuzungumza nae juu ya masuala mbalimbali kwa maslahi ya watu wa Ilemela na mkoa wa Mwanza kiujumla ambapo Mkuu huyo wa Mkoa amewahakikishia ushirikiano na utayari wa watu wake katika kufanikisha mradi huo huku akisisitiza kuwa hatamvumilia mtu yeyote mwenye malengo ovu ya kukwamisha utekelezaji wa mradi huo.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga ’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
02.11.2017
0 comments:
Post a Comment