Wananchi wanaoishi wilaya ya Ilemela wametakiwa kuunga mkono jitihada za utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazofanywa ndani ya wilaya yao kwa kushauri na kusaidia ufanikishaji wa miradi mbalimbali.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndg John Wanga akiwa kata ya Bugogwa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kwa kata za manispaa ya Ilemela anayoifanya kila baada ya miezi mitatu kwa kuambatana na wataalamu wa manispaa yake na viongozi mbalimbali kwenda kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi wa papo kwa hapo baadhi ya changamoto na kero zinazowakabili wananchi
‘… Ndugu zangu wananchi sisi tusiseme sana juu ya mafanikio ya miradi tunayoitekeleza lakini pia tunategemea mengi tusikilize kutoka kwenu, mtuambie, tushauriane, Tusiishie kulalamika tu kwasababu mnaweza mkatushauri pia kwamba sisi tunafikiri tukifanya hivi tunaweza tukaboresha zaidi …’ Alisema
Aidha mkurugenzi Wanga ametaja miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kwa kata ya Bugogwa ikiwemo zoezi la urasimishaji makazi, ujenzi wa majengo ya zahanati ya Karume katika kuhakikisha huduma za afya na huduma za mama na mtoto zinaimarika pamoja na mradi mkubwa wa usambazaji maji unaoendelea na kuwafafanulia juu ya hatma ya mradi wa umeme wa vijijini REA unaoendelea kutekelezwa katika vijiji vya kata hiyo.
Aliwasihi kumuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muumgano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, Mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula na madiwani kwa namna wanavyosimamia na kusaidia ufanikishaji wa miradi hiyo na kuahidi mifuko ya Saruji na Nondo za ujenzi wa daraja kwa wananchi wa mtaa Igombe B kama watachangia mawe ya ujenzi huo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Bugogwa Mhe William Mashamaba mbali na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo katika kata yake amewahakikishia ushirikiano katika kuhakikisha inafanikiwa tena kwa wakati huku akiwataka wananchi wake kufuata sheria na taratibu ili kujiepusha na usumbufu usiokuwa wa lazima.
Akihitimisha mkutano wa ziara hiyo mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela na diwani wa kata jirani na Bugogwa ya Sangabuye Mhe Renatus Mulunga amewakumbusha wananchi hao juu ya umuhimu wa kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo utaratibu wa Manispaa yake wa kusaidia kumalizia miradi inayoanzishwa na wananchi wenyewe huku akitolea mfano wa kuezekwa kwa msaada wa manispaa kwa jengo litakalokuwa limefikia hatua ya boma litakalojengwa kwa nguvu za wananchi
" Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga "
0 comments:
Post a Comment