Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya
pamoja na Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango wakimsikiliza kwa
makini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akitoa
maelezo ya ujio wa ugeni huo kuwa ni neema kwa nchi ya Tanzania kwani
Umoja wa Ulaya wametoa msaada wa Euro Milioni 50 utasaidia vijijini 3600
nchini kupata umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James (kulia) na akimweleza jambo Kamishna wa
Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica
wakati wa hafla fupi ya Umoja wa Ulaya (EU) kutiliana saini makubaliano
ya msaada wa Euro milioni 50 kwa ajili ya kusaidia usambazi wa umeme
vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza umeme Vijijini (REA).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James akiwa pamoja na Kamishna wa Ushirikiano wa
Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica wakisaini
Mkataba wa msaada wa fedha za kusaidia usambazaji wa umeme Vijijini
(EURO milioni 50) katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini
Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na
Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica, wakibadilishana hati za
makubaliano ya msaada wa ruzuku ya kiasi cha EURO Milioni 50 katika
ukumbi wa wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James akiwa na Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na
Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya
pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa msaada wa utekelezaji wa nishati
ya umeme vijijini katika ukumbi wa Wizara ya fedha na Mipango, Jijini
Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James akiagana na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa
na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica, baada ya kusaini
mkataba wa msaada wa Euro milioni 50 ambazo Umoja huo umeipatia Tanzania
kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini
REA.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango
………………
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
TANZANIA imezidi kupata neema
kutoka Jumuiya ya Kimataifa ambapo Novemba 2, 2017, Umoja wa Ulaya (EU)
umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 50, takriban Shilingi bilioni
130 kwa ajili ya kufadhili Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini
unaoendeshwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mkataba wa Makubaliano hayo
umetiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu
wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Kamishna wa
Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven
Mimica.
Msaada huo umelenga kuwasaidia
raia wa Tanzania kufikiwa na huduma nafuu ya nishati ya umeme kwa
kupanua uwezo wa gridi ya Taifa pamoja na mtandao wa usambazaji umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa
utakaoiwezesha nchi kuwa na umeme wa uhakika utakaochangia ukuaji wa
uchumi wa nchi na maendeleo ya watu wake.
“Umoja wa ulaya ni wadau wetu
muhimu wa maendeleo kutokana na misaada muhimu na mikubwa wanayotupatia,
na kusadia agenda yetu ya maendeleo” alisema Bw. James
Alisema kuwa kiasi cha msaada wa
Euro milioni 50 kilichotolewa na Umoja huo bila masharti yoyote si
kidogo, na kwamba kitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa
nishati ya umeme utakaochangia kuimarika kwa sekta ya viwanda
itakayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Bw. Doto James alisema kuwa tangu
Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini REA uanze miaka 9 iliyopita,
idadi ya vijiji vilivyounganishiwa umeme imeongezeka kutoka vijiji 400
mwaka 2008 hadi kufikia vijiji 4395 hivi sasa.
Alisema kuwa ni matarajio ya
Serikali kwamba ifikapo mwaka 2020, vijiji vyote 12,000 hapa nchini
vitakuwa vimeunganishwa na nishati hiyo hivyo kuchochea shughuli za
uzalishaji viwandani na kiuchumi kwa wananchi, vitaimarika.
Kwa upande wake, Kamishna wa
Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven
Mimica, amesema kuwa msaada huo wa Euro milioni 50 wanaoutoa ni sehemu
ya msaada wa Euro milioni 207 ambazo wanachama wengine wa Umoja huo,
ikiwemo Sweden, Uingereza, Norway na Benki ya Dunia, watatoa kufanikisha
mradi huo wa usambazaji umeme vijijini kupitia REA.
“Nguvu hizi za pamoja
zitaviwezesha takriban vijiji 3,600 vilivyoko maeneo mbalimbali ya nchi
ambapo watu zaidi ya milioni 1 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo”
Alisema Bw. Mimica
Alisema hatua hiyo itachangia
kuimarika kwa ubora wa maisha ya wananchi wa Tanzania, kuimarika kwa
sekta za afya, elimu na kuleta faida za kijamii na kiuchumi
zinazoonekana kwao moja kwa moja hususan wanawake na watoto.
Misaada ya Umoja wa Ulaya kwa
Tanzania imejikita katika Nyanja tatu za Utawala bora, Umeme na Kilimo
endelevu ambapo Umoja huo kupitia Mfuko wake wa Maendeleo (EDF) umetenga
kiasi cha Euro milioni 626 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014-2020
0 comments:
Post a Comment