METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 17, 2017

SERIKALI YATOA MAFUNZO KWA VIJANA ZAIDI YA 11,000


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweza kutoa mafunzo kwa vijana 11,492 katika fani mbalimbali kupitia vyuo vya umma, binafsi na makampuni ikiwa ni utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi.

Amesema programu hiyo ambayo ilianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2016/17, inalenga kuweka maeneo mahususi ya kuwezesha vijana wawe na ujuzi stahiki wa kuajirika au kujiajiri katika soko la ajira la ndani na la nje ya nchi.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 17, 2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, mwakani.

Amesema katika kutekeleza programu hiyo, Serikali imejikita katika maeneo ya kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi (apprenticeship); kutoa mafunzo ya ujuzi na uzoefu kazini (internship) kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo hususan wale wa vyuo vikuu; kutoa mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo; na kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.

Waziri Mkuu amesema katika kujenga ujuzi wa vijana kushiriki kwenye shughuli za kilimo, Serikali imeandaa mafunzo maalum ambayo yataanza rasmi Desemba, 2017 katika Halmashauri zote zilizowasilisha maombi.

“Tumeshirikisha Wakuu wa Mikoa yote na kuwaelekeza waandae maeneo ya kujifunzia vijana hao kwenye Halmashauri zote za mikoa yao,” amesema.

Amesema ofisi yake imepokea maombi ya kushiriki kutekeleza programu ya kukuza ujuzi katika eneo la kilimo kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Green House) kutoka mikoa mitano ya Kagera, Manyara, Ruvuma, Kilimanjaro na Shinyanga. “Ofisi yangu imefika katika Halmashauri zote za mikoa hii ili kujiridhisha kuwa imetenga maeneo kwa ajili ya kujenga vitalu vyumba vya kufundishia,” ameongeza.

Amesema katika mwaka huu wa fedha (2017/18), Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imetoa fursa za mafunzo mbalimbali ya vitendo kupitia Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kukubaliana kuwa ifikapo Desemba, 2017 vijana wote wawe wamepatiwa fursa za mafunzo katika maeneo ya kazi.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa viwanda na taasisi mbalimbali zishirikiane na Serikali kuwapa nafasi kwa vijana ili wajifunze kwa vitendo katika maeneo ya kazi  na kupata uzoefu  na ujuzi stahiki.

“Tuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu walioomba kushiriki mafunzo ya vitendo na kupata uzoefu wa kazi. Natoa wito kwa waajiri watoe nafasi kwa vijana wetu hawa kujifunza kwa vitendo. Serikali itaendelea kugharamia mahitaji ya msingi ya vijana hawa wakati wa mafunzo hayo,” amesisitiza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, NOVEMBA 17, 2017    
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com