METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 17, 2017

SERIKALI YAKARABATI VYUO 10 KWA SH. BILIONI 12

 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh. bilioni 11.9 kufanya ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na mabweni katika vyuo 10 vya ualimu nchini.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea, Tukuyu, Marangu, Kleruu, Korogwe na Tabora. “Ukarabati huu umewezesha wanachuo 5,920 waliokuwa wanasoma Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Dodoma kuhamishiwa katika vyuo hivyo,” ameongeza.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 17, 2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, mwakani.

Amesema ili kuongeza fursa za wanafunzi kusomea ualimu, Serikali imepanga kujenga na kukarabati vyuo vya ualimu vya Kitangali, Ndala, Mpuguso na Shinyanga kwa thamani ya sh. bilioni 36.47. 

Amesema mradi huo ambao utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016/2017 - 2018/2019, unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya ualimu.

“Ujenzi na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 katika mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya Serikali. Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na Ilonga.

Amesema vyuo vya ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda vitalazimika kujengwa upya baada ya wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai kukarabatiwa kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema ili kukabiliana na upungufu wa wahadhiri kwenye vyuo vya elimu ya juu, katika mwaka 2017/18, Serikali imepanga kusomesha wahadhiri 100 katika ngazi za shahada za umahiri na uzamivu.

Waziri Mkuu amesema kati ya mwaka 2016/17 na 2017/18, Serikali imeratibu upatikanaji wa wanafunzi wa Kitanzania wanaofadhiliwa kusoma nchi za nje ambapo China wapo wanafunzi 86, Uingereza (17), Misri (4), Korea (3), Urusi (13) na Thailand (2) huku baadhi ya wanufaika wakiwa ni wahadhiri wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.

Vilevile, kupitia kuimarika kwa mahusiano yetu ya kidiplomasia, Waziri Mkuu amesema, Septemba, mwaka huu, Serikali ilitia saini makubaliano na nchi ya Hungary ambapo itakuwa inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 30 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanza mwaka 2018/2019.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, NOVEMBA 17, 2017    
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com