Serikali imewaagiza wakurugenzi wa
Halmashauri kuwachukulia hatua wakandarasi wa maji wanaokiuka mikataba
walioingia kwa kuchelewa kutekeleza miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini Mendrad Lutengano Kigola juu
ya lini Serikali itamaliza kujenga mradi wa Kata ya Mtwango katika
Vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufana na Kibao.
“Viijiji vya Sawala, Mtwango, Rufana na
Kibao katika kata ya Mtwango ni miongoni mwa vijiji 12
vilivyopendekezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kupatiwa huduma ya
maji kupitia programu ndogo ya maji na usafi wa mazingira
vijijjini,” alisema Awezo.
Aliendelea kwa kusema, utekelezaji wa
mradi huo ulianza Juni 01, 2015 na ulitakiwa kukamilika Juni 01, 2016
kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.36 ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni
ujenzi wa miundombinu ya maji katika kijiji cha Sawala pekee ambapo hadi
sasa ujenzi umefikia asilimia 50.
“Hadi mwezi Novemba, 2016 mkandarasi
alikuwa hajakamilisha kazi na hivyo Halmashauri kuamua kuvunja mkataba
na halmashauri ilitangaza upya zabuni kwa ajili ya ukamilishaji wa kazi
zilizobaki,” alifafanua Aweso.
Amesema kuwa, mkandarasi mwingine
amepatikana na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Desemba, 2017
kwa muda wa miezi 12 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.81.
Kutokana na ucheleweshaji wa mradi huo,
Aweso amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwachukulia
hatua wakandarasi wa maji ambao hawatekelezi miradi yao kwa muda
uliopangwa ambao kwa kiasi kikubwa unawaathiri wananchi wanaohitaji
huduma ya maji kutokana na mradi kutekelezwa kwa muda mrefu.
Na Lilian Lundo, Dodoma
Chanzo:Dewjiblog
0 comments:
Post a Comment