Serikali imesema lugha ya Kiswahili ndio
lugha ambayo inatambulisha watanzania hivyo ni wajibu kwa wananchi
kutumia lugha hiyo kwa usahihi katika shughuli zao za ndani na nje ya
Taifa ili kukikuza na kukiendeleza .
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe alipokua akizungumza
katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Luninga ya Taifa
ambapo amesema ameliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuandaa
na kuwasilisha kwake orodha ya wahitimu wa lugha hiyo ili Serikali
iwatambue.
“Lugha ya Kiswahili ni lugha ya 10 kati
ya 6000 hapa duniani ni lazima watanzania waone umuhimu wa kutumia lugha
hii kwakua inatoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa nchi ambazo
zinahitaji wataalamu wa lugha hiyo,”alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha Dkt Mwakyembe ameeleza kuwa Sheria
ya Habari imeanza kutekelezwa na vyombo vingi vya habari na wanatasnia
kwa ujumla wameeilewa Sheria hiyo inayoeleza kuwa uhuru wa kutoa na
kupokea habari una mipaka na ni vyema wananchi wakaelewa kuwa mitandao
ya kijamii sio vyombo vya habari bali ni vyombo vya kutoa taarifa.
Hata hivyo Dkt. Waziri amesema vyombo
vya habari havikatazwi kuikosoa Serikali lakini vinatakiwa kukosoa kwa
hoja na si kuandika habari za uongo ambazo hazizingatii weledi na
taaluma ya habari.
Akizungumzia usikivu wa Shirika la
Utangazaji la Taifa Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali inaendelea na
jitihada za kuhakikisha usikivu wa matangazo ya Shirika hilo yanawafikia
wananchi wengi zaidi,na kwa upande wa Luninga tayari inapatikana katika
visimbuzi vyote.
Mhe Waziri ameongeza kuwa Mkataba kati
ya Shirika hilo la Utangazaji la Taifa na Kampuni ya StarTimes umeanza
kuangaliwa upya na taarifa itakapokamilika itawasilishwa kwa ajili ya
hatua zinazofuata.
“Kuna kamati imeundwa kuchunguza Mkataba
kati ya TBC na StarTimes na hivi karibuni viongozi wa StarTimes
watakuja hapa nchini kwa ajili ya majadaliano,” aliongeza Dkt.
Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa Sekta zake
zote zinaendelea kufanya vizuri na sehemu ambazo zina changamoto
zimeanza kutafutiwa ufumbuzi kwa kiasi kikubwa ili kufikia azma ya
Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
Na Shamimu Nyaki – WHUSM
0 comments:
Post a Comment