Msafara wa magari ukiongozwa na pikipiki
zaidi ya tano ulitokea makao makuu ya Global Group Sinza Mori Dar, huku
Mshindi wa Shindano la Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba akiwa kwenye
gari la wazi aina ya BMW huku mke wake akiwa kwenye gari lingine na
watoto wao .
Msafara ulipita Barabara ya Shekilango,
ukaingia Barabara ya Ali Hassani Mwinyi kisha ukaingia New Bagamoyo,
njiani kwa kuwa kulikuwa na gari la matangazo, watu walikuwa wamejipanga
kumshuhudi Majaba aliyejawa na tabasamu akipita akiwa kwenye gari hilo
la wazi.
Msafara ulipofika Tegeta umati ulikuwa
mkubwa na wengi waliokuwa wakimuona Majaba walikuwa hawaamini macho yao
kwani yeye mshindi alikuwa akiwapungua mkono na msafara ukawa unaenda
kwa mwendo wa polepole, hali iliyofanya baadhi ya wananchi kumkaribia
mshindi na walisikika wakisema ‘Hongera, Hongera!”
Lakini abiria waliokuwa kwenye mabasi ya
daladala nao walionekana wakitoa vichwa vyao madirishani na kumpongeza
Majaba ambaye mara zote alikuwa na tabasamu usoni.
Hali ilikua hivyo hivyo msafara
ulipofika Boko na baada ya kufika Bunju msafara ulisimama kabla ya
kuingia Barabara ya Mabwepande ambapo kwa mwendo mfupi tu msafara
uliingia kwenye nyumba mpya ya Majaba.
Mara baada ya kufika, Meneja Mkuu,
Abdallah Mrisho alitambulisha kwa wageni na wenyeji waliofika kushuhudia
makabidhiano hayo na kisha akampa nafasi Mkurugenzi Mtendaji wa Global
Group, Eric Shigongo kusema machache.
“Kifupi leo tunamkabidhi nyumba yake
Bwana Majaba. Ni jambo linalofurahisha kuona yupo hapa na familia yake
ya mke na watoto watatu, hivyo bila kupoteza muda karibuni tufungue
nyumba,” alisema Shigongo.
Baada ya kusema maneno hayo Shigongo,
Majaba na mkewe walishika utepe na Shigongo akaukata kuashirika kuwa
sasa wamekabidhiwa nyumba yao.
Baadaye Majaba na watu wengine
wakiongozwa na Shigongo waliingia ndani na kuoneshwa kila chumba,
baadaye nje na uani ambako kulikuwa na nafasi kubwa na Shigongo
alimuambia mke wa Majaba kwamba eneo hilo anaweza kufanyia miradi kama
ya kufuga.
Wenyeji walimkaribisha Majaba na baadaye
wakapiga picha ya pamoja huku wakimpongesha kwa kushinda nyumba hiyo.
Shughuli hiyo iliisha saa moja kasoro robo jioni.
HABARI NA ELVAN STAMBULI, PICHA MUSSA MATEJA.
0 comments:
Post a Comment