Mwanasiasa maarufu wa
Tanzania David Kafulila , pia Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), ambaye Disemba mwaka jana alijiunga na Chadema, David
Kafulila leo Jumatano Novemba 22,2017 ametangaza kujivua uanachama wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile alichosema hana
imani na vyama vya upinzani kama jukwaa salama la kupambana na ufisadi
nchini Tanzania.
Kafulila amejiondoa
CHADEMA na baada ya maamuzi hayo ameeleza sababu kwamba kwa sasa vyama
vya upinzani vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika juhudi zake za
kupambana na ufisadi na ghafla ufisadi siyo agenda kuu tena ya vyama vya
upinzani tena.
Kafulila ametoa waraka wa kujivua uanachama wa Chadema.
Katika waraka huo,
Kafulila amesema tangu Rais John Magufuli achaguliwe na kukabidhiwa
jukumu la kuongoza nchi, vita ya miaka mingi dhidi ya ufisadi imechukua
sura mpya.
“Wahusika na
watuhumiwa wakubwa wa rushwa ambao walikuwa hawaguswi huko nyuma
tunashuhudia wakifikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Kutokana na juhudi
za kupambana na rushwa na ufisadi zinazoendelea nchini,juhudi hizi
zinapaswa kuungwa mkono,”amesema Kafulila.
“Vyama vya
upinzani vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika juhudi zake za
kupambana na ufisadi. Ghafla ufisadi sio tena agenda kuu ya vyama vya
upinzani nchini, kwa sababu hii, ni wazi kuwa upinzani sio tena jukwaa
salama la kuendesha vita dhidi ya ufisadi,” ameongeza.
Kafulila ambaye ni
mme wa mbunge wa viti maalum Chadema, Jesca Kishoa amesema “kwa kuwa
sina imani tena na upinzani kama jukwaa salama la kupambana na ufisadi,
nimeamua kwa hiari na utashi wangu kujivua uanachama wa Chadema kuanzia
leo”,amesema Kafulila.
“Nitatangaza
katika siku za hivi karibuni jukwaa jipya la harakati zangu dhidi ya
ufisadi. Nawatakia safari njema waliobaki ndani ya Chadema kwa kile
wanachokiamini”,amesema.
Kafulila aliyekuwa
mbunge 2010-2015 alitikisa kwenye mapambano ya sakata la ufisadi wa
mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow iliyoitikisa serikali katika
utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ametangaza uamuzi huo leo Novemba
22,2017.
0 comments:
Post a Comment