METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 25, 2017

WATUMISHI 28 WAFUKUZWA HALMASHAURI YA MJI WA KIBAHA KWA MAKOSA YA KINIDHAMU-SOZI

Mkuu wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,wa pili kushoto ,katibu tawala wilaya ya Kibaha Sozi Ngate wa kwanza kulia ,pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Leonard Mloe wa pili kutoka kulia ,wakiwa wameshika tuzo ya kuwa wa kwanza katika ufungaji wa mahesabu ya serikali kati ya halmashauri zote nchini mwaka 2014/2015  iliyopatiwa halmashauri hiyo
Picha na Mwamvua Mwinyi
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha,mkoani Pwani,imewachukulia hatua ya kinidhamu kwa kuwafukuza kazi watumishi 28 kwa makosa ya utoro kazini,kughushi vyeti na upotevu wa mali za halmashauri.
Aidha halmashauri hiyo ,inakabiliwa na upungufu wa watumishi 164,ambapo uhaba mkubwa upo katika idara ya utawala ,maji na afya.
Licha ya upungufu huo,halmashauri hiyo imekua ya kwanza katika ufungaji wa mahesabu ya serikali kwa mwaka 2014-2015 kati ya halmashauri 186 nchini.
Hayo aliyasema katibu tawala wa wilaya ya Kibaha,Sozi Ngate kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo,wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya halmashauri hiyo katika ziara ya siku moja ya mkuu wa mkoa wa Pwani,:’Alipotembelea baadhi ya miradi ikiwemo kituo cha mabasi cha kisasa kitakachogharimu bilioni 3.4 na ujenzi wa jengo la halmashauri hiyo.
Sozi alisema ,kati ya watumishi waliofukuzwa kazi ni pamoja na walimu 20,watendaji watatu,tabibu wawili,katibu muhtasi ,afisa ardhi na daktari mmoja.
Hata hivyo alieleza,ili kukabiliana na upungufu wa watumishi halmashauri inategemea kuajiri watumishi 73 ambao mishahara yao imetengwa na ofisi ya rais –utumishi na wizara ya fedha na mipango kwa mwaka 2017/2018.
Akielezea zoezi la uhakiki wa vyeti vya elimu,,Sozi alieleza ulifanyika kwa watumishi wote 1,529 ambapo watumishi 73 wameondolewa kwa kukutwa na vyeti feki.
“Kwa upande wa uhakiki wa watumishi hewa ulianzia machi 2016 hadi april,jumla ya watumishi 20 waligundulika ni watumishi hewa na jumla ya fedha mil 19.161.557 ziliokolewa”alifafanua Sozi.
KATIKA HATUA NYINGINE,akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo ,alisema wanaendelea kusimamia ukusanyaji huo .
Sozi alisema mwaka 2016-2017 halmashauri ilikadiria kukusanya zaidi ya sh.bil.3.954.4 katika vyanzo vya ndani na makusanyo halisi hadi kufikia juni 30 mwaka huu ilifanikiwa kukusanya sh.bil.3.671.950.5 sawa na asilimia 93.
Mwaka 2017-2018 halmashauri ya mji huo imekisia kukusanya sh.bil.3.705.549 ambapo mapato halisi hadi septemba 30 ,2017 imekusanya sh.bil.1.431.090.552 sawa na asilimia 38.6 ya makisio.
“Tusipojisifu wenyewe hakuna wa kutusifia,tujipongeze halmashauri yetu imekuwa ya kwanza katika ufungaji wa mahesabu ya serikali kwa mwaka 2014-2015 kati ya halmashauri zote nchini ,
VIWANDA….Halmashauri ya mji Kibaha inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ambapo katika robo ya kwanza ya 2017/2018 imeweza kutumia mil.100 kufungua barabara eneo la viwanda Zegereni na inaendelea kupokea maombi ya wawekezaji.
Sozi alielezea,mji huo una jumla ya viwanda 119 vinavyofanya kazi kati ya hivyo vikubwa ni vitano,vya kati 16 na vidogo 98 huku viwanda vinne vinaendelea kujengwa .HATA HIVYO ,kuhusu soko jipya la Mnarani (Loliondo)alisema zimeshawekwa taa na wameshatenga eneo la kujengwa kituo cha polisi .
MKUU WA MKOA WA PWANI,mhandisi Evarist Ndikilo ,aliipongeza halmashauri hiyo kwa jitihada mbalimbali wanazozifanya kimaendeleo.Alisema anaendelea kufuatilia maombi ya halmashauri hiyo ya mji kuwa manispaa ambayo yalishayapelekwa TAMISEMI .
Mhandisi Ndikilo alisema ,mji huo unakua siku hadi siku,huduma za kijamii zinaongezeka,idadi ya watu imeongezeka hivyo vigezo vya mji kuwa manispaa vimeshafikiwa.“Mkoa wa Pwani unaongoza katika kukuza uchumi wa viwanda ,nawaombeni tuongeze jitihada kuboresha miundombinu ya maji,barabara na umeme kuvutia wawekezaji zaidi ya sasa”alifafanua mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo,aliitaka halmashauri hiyo kuweka ulinzi kwenye soko la Mnarani ili kulinda mali zao sokoni hapo.Alisema kuna kila sababu ya kuweka mikakati ya muda mrefu na mfupi ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara usiku kwa ajili ya ulinzi, kuwasaidia watu na mali zao.
Katika ziara yake mhandisi Ndikilo,alitembelea ujenzi wa jengo la ofisi za halmashauri hiyo na kituo cha mabus kipya kinachojengwa eneo la CBD kitakachogharimu bilioni 3.4 hadi kukamilika.
NAE meneja wa kampuni ya Group Six International Ltd ,inayojenga kituo cha hicho ambayo ilijenga stendi ya kisasa ya Msamvu mkoani Morogoro,mhandisi Chen Xlong ,alisema ujenzi umefikia asilimia 45.
Alisema licha ya kuwa nyuma kidogo ya wakati katika kukamilisha ujenzi huo lakini wanatarajia kukamilisha ujenzi huo desemba mwaka huu.
Stendi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 60 kwa wakati mmoja na inajengwa kwa ufadhili wa bank ya dunia kupitia fedha za ruzuku kwenye mradi wa uendelezaji wa miji (ULGSP) unaoendeshwa kwenye miji 18 hapa nchini ikiwemo Mji wa Kibaha
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com