Wanawake wanaendesha malori, mabasi, treni na
ndege, ni makondakta wa daladala na shughuli nyingine ambazo awali
zilidhaniwa kuwa zinawafaa wanaume pekee.
Kazi pekee
inayoonekana pengine kuwa rahisi, kuendesha gari ndogo za abiria, yaani
teksi kwa kuwa ni kawaida kuwaona wanawake, hata wasichana wadogo
wakiendesha vyombo hivyo.
Hiyo ilikuwa nadra sana kwa mwanamke kuendesha teksi ambazo hufanya kazi hadi usiku mwingi.
Lakini,
jijini Dar es Salaam mwiko huo umeshakoma; wanawake sasa ni madereva wa
magari hayo madogo ya abiria, lakini wakiwa wamewezeshwa na kampuni ya
Uber iliyorahisisha huduma ya usafiri kwa kutumia teknolojia ya simu.
Na wanawake hao ni mchanganyiko; kuanzia wasomi hadi wenye elimu ya kawaida.
“Wakati
nikiwa Nairobi, nilitumia app ya Uber. Niliipakua kwenye simu yangu na
mtu ambaye alikuja kunichukua (kwa gari) alikuwa mwanamke,” alisema Suma
Mwaitenda (34), mthamini na mhadhiri wa Chuo Kikuu Ardhi ambaye sasa ni
dereva wa Uber.
“Nilivutiwa na ujasiri wake. Mwanamke
yule alinieleza uzoefu wake na aliingiaje katika shughuli ya Uber.
Alisema waliwahi kuajiriwa lakini akaacha kazi baada ya kuona fursa ya
Uber.”
Suma, ambaye alikuwa akizungumza na Esther
Kibakaya wa gazeti la The Citizen, alisema alihamasika na kuamua kwamba
akirejea Tanzania angewashirikisha wenzake, hasa wanawake kuhusu fursa
hiyo.
“Nilijiambia kuwa kama nataka watu waamini kuwa
inawezekana, lazima niwe wa kwanza kufanya hilo,” alisema Suma, ambaye
ni ofisa mtendaji wa taasisi ya Uhuru Women Club.
Suma anamudu kufanya kazi hiyo pamoja na ya uhadhiri na kulea familia yake.
“Kwa
kawaida ninatenga saa tatu hadi nne kwa siku kulingana na ratiba yangu
ya kufundisha. Wakati mwingine naweza kuwa ninatakiwa kufundisha chuoni
asubuhi hadi mchana kwa hiyo napata muda saa 10:00 jioni,” alisema.
“Kama
ikitokea nina miadi mjini, basi nawasha app ya Uber ili nichukue abiria
kama inavyokuwa naporejea. Kwa kifupi nafanya kazi hii kadri navyopata
muda,” alisema Suma.
Suma hakuanza kazi hiyo kinyemela; alimshirikisha mumewe na ilichukua muda mrefu kumshawishi hadi kukubali.
Anasema
kazi hiyo ina changamoto zake kama zilivyo nyingine, kubwa ikiwamo ya
kutongozwa na abiria, lakini anasema anaweza kukabiliana nazo.
Suma anashauri wanawake wenzake waone fursa ya kutumia magari yao kibiashara badala ya kuyaacha yakae bila ya shughuli zozote.
Suma si mwanamke pekee aliyeingia kwenye biashara hiyo.
Happiness
Mremi, mhitimu wa shahada ya elimu katika Chuo Kuu cha St Augustine,
Angelina Shonza, aliyehitimu shahada ya ustawi wa jamii, Pascalia
Dominic na Prisca Kabendera ni baadhi tu ya wanawake wanaofanya kazi
hiyo.
Baada ya kumaliza masomo yake mwaka 2015,
Happiness alianza kujishughulisha na kilimo cha mpunga mkoani Mwanza na
baadaye biashara ya nguo eneo la Kariakoo, lakini mambo hayakwenda
vizuri.
“Ilikuwa ni wakati huo nilipomsikia mmoja wa marafiki wa familia aliyetutembelea akizungumzia Uber,” alisema Happiness.
“Nilimwambia
mume wangu na akanieleza jinsi biashara ilivyo. Nilipomwambia kuwa
nataka nifanye, alinijibu kuwa siwezi kufanya kitu kama hicho,” alisema
Happiness.
“Nilifanya uchunguzi na kufurahia zaidi wazo
hilo na kumwambia mume wangu kuwa nataka kuwa dereva wa Uber kwa sababu
gari langu linaegeshwa tu nyumbani bila ya kazi. Alikataa kabisa,
ikafika wakati ikawa kila nikitaja Uber kunazuka majibizano makali.”
Baadaye alifanikiwa kumshawishi baada ya kwanza kutembelea ofisi za Uber na kuonyeshwa jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.
Naye
Shonza anasema wazo la kukaa bila ya kazi wakati kulikuwa na kitu
ambacho angeweza kufanya kupata fedha, ndilo lililomsukuma kuwa dereva
wa Uber.
“Mtu wa kwanza kumwambia alikuwa mume wangu,
lakini aliniambia si kazi nzuri kwa mwanamke kwa sababu ni kazi ngumu
kushinda usiku mzima umekaa ukiendesha gari.
“Hata
hivyo, hilo halikunizuia kujaribu. Nilijaribu na baadaye kuanza kazi
kama dereva kamili, nikifanya kazi kuanzia saa 10:00 au saa 11:00
alfajiri hadi saa 2:00 usiku,” alisema Shonza.
Shonza
ameshafanya kazi hiyo kwa miezi mitano sasa na hajutii uamuzi wake,
akiwa anajipatia Sh2 milioni hadi 2.5 milioni kwa mwezi.
0 comments:
Post a Comment