METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 1, 2017

Wanawake wasomi madereva wa teksi Dar

By Mwandishi Wetu, Mwananchi
 
Wanawake wanaendesha malori, mabasi, treni na ndege, ni makondakta wa daladala na shughuli nyingine ambazo awali zilidhaniwa kuwa zinawafaa wanaume pekee.
Kazi pekee inayoonekana pengine kuwa rahisi, kuendesha gari ndogo za abiria, yaani teksi kwa kuwa ni kawaida kuwaona wanawake, hata wasichana wadogo wakiendesha vyombo hivyo.
Hiyo ilikuwa nadra sana kwa mwanamke kuendesha teksi ambazo hufanya kazi hadi usiku mwingi.
Lakini, jijini Dar es Salaam mwiko huo umeshakoma; wanawake sasa ni madereva wa magari hayo madogo ya abiria, lakini wakiwa wamewezeshwa na kampuni ya Uber iliyorahisisha huduma ya usafiri kwa kutumia teknolojia ya simu.
Na wanawake hao ni mchanganyiko; kuanzia wasomi hadi wenye elimu ya kawaida.
“Wakati nikiwa Nairobi, nilitumia app ya Uber. Niliipakua kwenye simu yangu na mtu ambaye alikuja kunichukua (kwa gari) alikuwa mwanamke,” alisema Suma Mwaitenda (34), mthamini na mhadhiri wa Chuo Kikuu Ardhi ambaye sasa ni dereva wa Uber.
“Nilivutiwa na ujasiri wake. Mwanamke yule alinieleza uzoefu wake na aliingiaje katika shughuli ya Uber. Alisema waliwahi kuajiriwa lakini akaacha kazi baada ya kuona fursa ya Uber.”
Suma, ambaye alikuwa akizungumza na Esther Kibakaya wa gazeti la The Citizen, alisema alihamasika na kuamua kwamba akirejea Tanzania angewashirikisha wenzake, hasa wanawake kuhusu fursa hiyo.
“Nilijiambia kuwa kama nataka watu waamini kuwa inawezekana, lazima niwe wa kwanza kufanya hilo,” alisema Suma, ambaye ni ofisa mtendaji wa taasisi ya Uhuru Women Club.
Suma anamudu kufanya kazi hiyo pamoja na ya uhadhiri na kulea familia yake.
“Kwa kawaida ninatenga saa tatu hadi nne kwa siku kulingana na ratiba yangu ya kufundisha. Wakati mwingine naweza kuwa ninatakiwa kufundisha chuoni asubuhi hadi mchana kwa hiyo napata muda saa 10:00 jioni,” alisema.
“Kama ikitokea nina miadi mjini, basi nawasha app ya Uber ili nichukue abiria kama inavyokuwa naporejea. Kwa kifupi nafanya kazi hii kadri navyopata muda,” alisema Suma.
Suma hakuanza kazi hiyo kinyemela; alimshirikisha mumewe na ilichukua muda mrefu kumshawishi hadi kukubali.
Anasema kazi hiyo ina changamoto zake kama zilivyo nyingine, kubwa ikiwamo ya kutongozwa na abiria, lakini anasema anaweza kukabiliana nazo.
Suma anashauri wanawake wenzake waone fursa ya kutumia magari yao kibiashara badala ya kuyaacha yakae bila ya shughuli zozote.
Suma si mwanamke pekee aliyeingia kwenye biashara hiyo.
Happiness Mremi, mhitimu wa shahada ya elimu katika Chuo Kuu cha St Augustine, Angelina Shonza, aliyehitimu shahada ya ustawi wa jamii, Pascalia Dominic na Prisca Kabendera ni baadhi tu ya wanawake wanaofanya kazi hiyo.
Baada ya kumaliza masomo yake mwaka 2015, Happiness alianza kujishughulisha na kilimo cha mpunga mkoani Mwanza na baadaye biashara ya nguo eneo la Kariakoo, lakini mambo hayakwenda vizuri.
“Ilikuwa ni wakati huo nilipomsikia mmoja wa marafiki wa familia aliyetutembelea akizungumzia Uber,” alisema Happiness.
“Nilimwambia mume wangu na akanieleza jinsi biashara ilivyo. Nilipomwambia kuwa nataka nifanye, alinijibu kuwa siwezi kufanya kitu kama hicho,” alisema Happiness.
“Nilifanya uchunguzi na kufurahia zaidi wazo hilo na kumwambia mume wangu kuwa nataka kuwa dereva wa Uber kwa sababu gari langu linaegeshwa tu nyumbani bila ya kazi. Alikataa kabisa, ikafika wakati ikawa kila nikitaja Uber kunazuka majibizano makali.”
Baadaye alifanikiwa kumshawishi baada ya kwanza kutembelea ofisi za Uber na kuonyeshwa jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.
Naye Shonza anasema wazo la kukaa bila ya kazi wakati kulikuwa na kitu ambacho angeweza kufanya kupata fedha, ndilo lililomsukuma kuwa dereva wa Uber.
“Mtu wa kwanza kumwambia alikuwa mume wangu, lakini aliniambia si kazi nzuri kwa mwanamke kwa sababu ni kazi ngumu kushinda usiku mzima umekaa ukiendesha gari.
“Hata hivyo, hilo halikunizuia kujaribu. Nilijaribu na baadaye kuanza kazi kama dereva kamili, nikifanya kazi kuanzia saa 10:00 au saa 11:00 alfajiri hadi saa 2:00 usiku,” alisema Shonza.
Shonza ameshafanya kazi hiyo kwa miezi mitano sasa na hajutii uamuzi wake, akiwa anajipatia Sh2 milioni hadi 2.5 milioni kwa mwezi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com