Siku chache zilizopita, taarifa za kusikitisha
katika sekta ya elimu ziliibukia wilayani Mkuranga ambako baadhi ya wana
jamii wameshindwa kudhibiti uwapo wa mila hatarishi zinazochangia
mdondoko wa wanafunzi wa kike.
Takwimu zinaonyesha
wanafunzi 7,151 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2011 wilayani
humo waliotarajiwa kuhitimu mwaka huu kati yao 963 walikatisha masomo.
Hata
hivyo, mila inayolalamikiwa kudidimiza elimu wilayani humo ya wasichana
wengi kuchezwa ngoma imegeuka kuwa kikwazo na miongoni mwao huishia
kufanya majaribio ya mafunzo wanayopewa unyagoni na matokeo yake huacha
shule.
“Mwanafunzi anapopelekwa kwenye unyago akili
yake inabadilika, ni wachache sana ambao wanaweza kurudisha mawazo yao
darasani, wengi wanafikiria jinsi ya kuyafanyia kazi mafunzo
waliyoyapata,” anasema mdau wa elimu, Tabia Mohamed.
Ofisa
Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Peter Nambunga alieleza kuwa
Serikali inaendelea kukabiliana na na suala hilo pamoja na lile la ngoma
za vidogoro vinavyofanyika nyakati za usiku vijijini. “Tumeliona hilo
na sio hilo pekee kuna suala la vigodoro, kuonyesha video haya yote
yanaleta changamoto ila tumeshawapelekea madiwani tunasubiri watunge
sheria,” anasema Nambunga
Katika mwendelezo huohuo wa
kupambana na ujinga mkoani Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happiness
Seneda amesema kwamba nao wapo nyuma kielimu baada ya kugundua idadi
kubwa ya wanafunzi wanapata sifuri kwenye mitihani ya kidato cha nne.
Seneda alisema hali ya elimu wilayani hapa inasikitisha, licha ya jitihada za Serikali kutilia mkazo suala la elimu bure nchini.
Alisema
mwaka 2016 wahitimu wa kidato cha nne walikuwa 960, lakini waliopata
sifuri walikuwa 457 huku mwaka 2015 kulikuwa na wahitimu 820 na
waliopata sifuri walikuwa 334, ilhali mwaka 2014 kulikuwa na sifuri 134.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ili kutatua tatizo hilo kuanzia kesho
kutakuwa na akaunti maalumu benki ambazo wadau wa elimu watatangaziwa
ili wachangie kuiboresha.
Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, Hamisi Dikupatile alisema fedha zitakazopatikana zitasadia watoto
waliopo kwenye kambi za kujisomea na kuboresha miundombinu ya elimu,
nyumba za walimu na vifaa vya kujifunzia.
0 comments:
Post a Comment