Matukio ya uhalifu yanayoendelea
nchini yamewaibua viongozi wa dini ambao licha ya kuelezea wasiwasi wao
kutokana na kuongezeka, wameitaka Serikali ibuni mikakati ambayo
itamhakikishia kila raia usalama wake.
Wamesema kuna
haja kwa wananchi kuhakikishiwa usalama kwani woga na hali ya
kutokuaminiana iliyoanza kujitokeza miongoni mwao inaweza kusababisha
hali kuwa mbaya baadaye.
Viongozi hao wamesema hayo
jana walipokutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba katika
kikao kilichofanyika jiji hapa na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia.
Ingawa kikao
hicho kilikuwa sehemu ya utamaduni wa viongozi wa dini zote kukutana na
kujadiliana kuhusu mambo yanayohusu nchi, lakini kwa sehemu kubwa
kilitawaliwa na matukio yaliyoanza kuibuka katika siku za hivi karibuni.
Matukio
hayo ni pamoja na kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu, vitisho vinavyotolewa kwa baadhi ya makundi ya
watu pamoja na tukio la kukutwa kwa miili katika eneo la Coco Beach
jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Askofu Alinikisa Cheyo alisema katika majadiliano hayo
wamekubaliana kwamba suala la ulinzi wa raia linapaswa kuwa ajenda ya
kudumu kwa Serikali bila kujali itikadi.
“Ni muhimu
mwanachi ahakikishiwe usalama wake popote pale alipo… potelea yukoje,
yuko wapi lakini ahakikishiwe ya kwamba yupo salama,” alisema.
Hii
ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wa dini kukutana na waziri Mwigulu
tangu kuibuka kwa matukio hayo na walitumia fursa hiyo kufanya maombi ya
pamoja kumuombea Lissu ambaye anaendelea na matibabu jijini Nairobi.
Sheikh
Hassan Said Chizenga kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania
(Bakwata) alisema mikutano ya namna hiyo inawapa fursa waumini wa pande
zote kubadilishana mawazo na kisha kukubaliana njia bora zaidi ya
kulinda amani ya nchi.
“Huku kukutana tu kwenyewe pia
kunasaidia kufuta tofauti zilizopo baina yetu na kuweza kutupa moyo wa
kushirikiana sisi kwa sisi na kujua mambo mengine ambayo tulikuwa
hatujui,” alisema.
Baadaye waziri Nchemba alimwambia
mwandishi wetu kuwa ingawa Serikali inaendelea kuchukua jukumu la
kuimarisha ulinzi na usalama, wananchi nao wanapaswa kuchukua tahadhari.
“Wananchi
lazima wawe makini maana unaweza ukamkuta mtu anamtuma mtoto kwenda
dukani nyakati za usiku wakati sasa kuna haya matukio ya utekaji watoto,
kwa hiyo wananchi lazima wazingatie hilo,” alisema.
Alisema
Serikali imezipokea hoja zilizotolewa na viongozi wa dini na kwa
kuzitilia maanani, inaanza kuangalia namna ya kufanikisha ulinzi wa
nyumba kumi.
“Wametupa changamoto na sisi tunazifanyia kazi na tunaangalia uwezekano wa kuanzisha ulinzi wa nyumba kumi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment