METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 10, 2017

TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI JUMANNE 10 OKTOBA 2017

Mapema April mwaka 2017 Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ulianza rasmi zoezi la Uchaguzi kwa mujibu wa Ratiba ya Uchaguzi ya  Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake. Kwa upande wa UVCCM chaguzi zilianza ngazi ya matawi na sasa zimefikia ngazi za Mkoa kuelekea kukamilika ngazi ya Taifa mwezi Novemba 2017.
 
Itakumbukwa kuwa tumekuwa tukitoa taarifa za mara kwa mara juu ya maendeleo ya Uchaguzi ndani ya jumuiya yetu ili kujenga uelewa,  kuwapa ufahamu na kutoa maelekezo yanayojenga mazingira bora ya uwazi,  mfumo shirikishi  na kuonyesha jinsi UVCCM ilivyojipanga katika kuonyesha ukomavu  wa demokrasia ndani ya  jumuiya yetu.
 
Hadi kufika Oktoba 10, 2017 jumla ya Matawi 23,398 sawa na asilimia 100%  yalikamilisha uchaguzi, Kata  4,036 sawa na asilimia 100% zimekamilisha uchaguzi, Majimbo 54 ya Zanzibar  sawa na asilimia 100% yamekamilisha uchaguzi, Wilaya zote 167 zimekamilisha uchaguzi sawa na asilimia 100%.
 
Nichukue fursa hii niwapongeze na kuwashukuru Vijana wote waliojitokeza kuomba nafasi mbali mbali kuanzia Tawi na Wilaya na niwapongeze pia kwa dhati kabisa wale wote ambao sasa wamechaguliwa kushika nafasi mbali mbali za uongozi kuanzia ngazi ya Matawi hadi Wilaya. Ni matumaini yetu baaada ya Uchaguzi kumalizika sasa vijana wote watakusanya nguvu zao ili kukipigania Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya yetu. 

Tuna matarajio kuwa sasa ni muda muafaka wa kujenga na kuimarisha misingi ya Umoja, Ushirikiano na Mshikamano katika maeneo yao kwa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa, Chama, na Jumuiya.
 
Tunaendelea kuwakumbusha Vijana wote kuwa Demokrasia ni jambo muhimu linalohitaji kuheshimiwa na kuenziwa ndani ya Chama na  Jumuiya zake. Ndio maana kila wakati tumekuwa tukisisitiza ulazima wa Kiongozi wa UVCCM mahali popote alipo achaguliwe kwa  kufanyika chaguzi huru na za haki, kuzingatia Kanuni na Taratibu kama zilivyoagizwa na vikao husika bila ya kukiuka, kupuuzwa au kuvunjwa.
 
Nia na azma ya UVCCM kujenga haiba mpya na njema inayoheshimu uhalisia wa misingi  ya demorasia ya kweli, kuendeleza utii, adabu, nidhamu, kuheshimu miiko na maadili kwa kila anayetaka aidha kuchagua au kuchaguliwa.
 
Misingi mikuu ya uendeshaji wa  Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake kama tunavyojua hutokana na matakwa ya Katiba, Kanuni, Taratibu na miongozo inayotolewa na Viongozi wake.

Tunaelewa na kufahamu hakuna kizuri kisichokosa kasoro au kukabiliwa na changamoto ndogo ndogo. Kwa wale wote ambao watakuwa na maoni, malalamiko au ushauri wa aina yoyote  tunawakumbusha kufuata taratibu za Kikanuni.
 
Kwa mujibu wa Kanuni ya Uchaguzi ya mwaka 2017 Uk.9 Ibara ya;

19.  nanukuu “ Mara baada ya matokeo kutangazwa
mgombea yeyote aliyekubaliwa katika uteuzi wa mwisho wa uchaguzi wa ngazi inayohusika endapo anayo malalamiko kuhusu uchaguzi huo atawasilisha malalamiko yake kwa kwa Katibu wa Vijana wa ngazi ya uchaguzi aliyoomba. Isipokuwa kama uchaguzi unaolalamikiwa ni uchaguzi wa ngazi ya Taifa malalamiko yatawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa CCM.

20. Malalamiko yatawasilishwa kwa maandishi, na lazima aonyeshe ni jinsi gani Kanuni za uchaguzi au Kanuni za Jumuiya zilivyokiukwa katika shughuli za uendeshaji wa Uchaguzi unaolalamikiwa.

Barua ya malalamiko ionyeshe wazi wazi jina na anuani ya mlalamikaji.

21.Malalamiko hayo itabidi yawasilishwe ndani ya siku kumi na Nne (14) tangu siku ya matokeo ya uchaguzi unaolalamikiwa ulipotangazwa. Tarehe ya kuwasilisha rufaa izingatie pia muhuri wa Posta kwa wale watakaoleta rufaa kwa njia ya Posta kwani malalamiko yanaweza kufika baada ya siku kumi na nne kupita.

22.Malalamiko yatakayowasilishwa kinyume na Kanuni hizi za uchaguzi hayatashughulikiwa.

Kwa maelezo hayo ya Kikanuni hakuna sababu kwa mtu yoyote kuendelea kutumia njia zisizo sahihi kutoa malalamiko, kukashifu wenziwe, kutoa taarifa za ndani za vikao aidha kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, ama njia nyingine yoyote kinyume na utaratibu na utamaduni wa CCM na Jumuiya zake.

Kwa upande wa ngazi ya Mikoa hadi kufika Oktoba 10 mwaka 2017 Mikoa 26 kati ya 32 imekamilisha  hatua ya kupitia majina ya wagombea wa nafasi mbali mbali na kuwasilisha katika ngazi husika ili kuendelea na utaratibu unaofuata kabla  hatua ya uteuzi kwa nafasi za uwakilishi katika vikao vya Kikatiba vya CCM.
 
Kwa upande wa wagombea ngazi ya Taifa mchakato wa vikao unatarajiwa kukamilika siku chache zijazo na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Chama ili kuendelea na utaratibu wa vikao vya Kikatiba vya Uteuzi.
 
Ngazi ya Taifa vijana  371 wamejitokeza kuomba nafasi mbali mbali za  uongozi ndani ya UVCCM ikiwemo kuwania nafasi ya Mwenyeikiti wa UVCCM Taifa, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe 5 wa Halmashauri Kuu ya Taifa, nafasi 3 Tanzania Bara na nafasi 2 Tanzania Zanzibar, Wajumbe 5 wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa nafasi 2 Tanzania Zanzibar  na 3 Tanzania Bara na nafasi za Uwakilishi toka Vijana kwenda UWT na Wazazi.
 
Baada kukamilika vikao vya Kamati za Utekelezaji UVCCM na Kamati za siasa za Mikoa, maandalizi kwa ajili vikao vya Kikanuni vya  ngazi ya Taifa  yanaendelea vyema, vikao  vyote vya UVCCM vinatarajiwa kufanyika kama ifuatavyo:-
 
Oktoba 11 hadi 12/2017  Sekretariet ya Baraza Kuu la  UVCCM Taifa.

OKTOBA  15 hadi 16/ 2017 Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa.

Oktoba 17/2017 Baraza Kuu la Umoja wa Vijana CCM Taifa.

Kwa wa wale  waliojaza fomu za kugombea Ngazi ya Taifa,  wanatakiwa kufika mbele ya  kikao cha Kamati ya Utekelezaji UVCCM Taifa siku ya Jumapili Oktoba 15 mwaka 2017 saa 4:00 Asubuhi  huku wakiwa na vielelezo vyote halisi ambavyo waliviambatanisha katika fomu zao.

Inasisitizwa ni wale waliojaza fomu tu za kuomba nafasi ndio wanaohitajika kufika Dodoma Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Taifa White House, hakuhitajiki wapambe, shangwe wala mikusanyiko ya aina yoyote muda wote wa vikao vya Kikanuni vikiendelea na baada ya vikao.
 
Tunaendelea kuwakumbusha na kuwasisitiza wale wote walioonyesha nia kwa kujaza fomu za kuomba uongozi ndani ya UVCCM, waheshimu  maelekezo ya Kikatiba, Kikakuni, wafuate taratibu na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara bila kwenda kinyume.

Hatutamvumilia wala kumstahimilia mtu yoyote kumchukulia hatua za kinidhamu, kimaadili na ikibidi za kisheria  ili kulinda heshima na haiba ya Umoja wa Vijana wa CCM. Kila mmoja atambue anafuatiliwa kwa karibu sana katika kubaini mambo yote yanayokwenda kinyume.
 
Wote yatupasa kuelewa kuwa kila jambo lina wakati wake, tutaendelea kutoa maelekezo na miongozo ya mara kwa mara kwa lengo la kuhuisha uwazi hasa kipindi hiki ambacho jumuiya inakwenda kupata viongozi wa kuiongoza kwa kipindi 2017/2022.
 
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunaendelea kusisitiza kuwa sifa na wasifu wa kila mgombea kwa kadri alivyojaza kwenye fomu yake,  utaandaliwa na kuandikwa vizuri katika Kitabu Maalum cha wagombea baada ya uteuzi kufanyika.
 
Kila mgombea atapata nafasi ya kujieleza, kujinadi ukumbini mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu, kutoa wasifu wake, kutaja dhamira na malengo  katika Mkutano Mkuu husika si kinyume na hivyo baada ya taratibu za vikao kukamilika. 

Tunaendelea kuwakumbusha tena kuwa kuanza kampeni mapema au wapambe kufanya usahabiki wa kisiasa, kumnadi kwa kuitisha vikao vya ushawishi, kumpigia debe, au kujipitisha pitisha na kuelezea nafasi anayogombea, akibainika kutampotezea sifa mgombea ya  kuteuliwa.
 
Ni marufuku na hairuhusiwi kabisa muda ukifika kwa mgombea yoyote kufanya kampeni za kihuni kwa kutumia lugha chafu, siasa za maji taka, matusi, dharau kinyume na ubinadamu pia kushiriki kejeli dhidi ya wenzake.
 
Ni mwiko kabisa kutumia makaratasi, vipeperushi au nembo yoyote yenye kuonyesha uhalisi wa mgombea katika uchaguzi huu.Ikiwa hayo yote yataachwa yafanyike bila ya kuyadhibiti  kuyaasa na kuyakemea ni mwanzo wa kukaribisha mvurugano, mgawanyiko na kujipenyeza kwa adui rushwa hivyo tunaendelea kuwaagiza watendaji wote wa ngazi husika kusimamia matakwa ya Kikanuni, Kimaadili na Kikatiba.
 
Tunaendelea kusisitiza Uchaguzi wa UVCCM katika ngazi zilizobakia zitafanyike  kwa njia huru na uwazi huku kila mgombea akipitishwa na vikao vya Kikanuni vya jumuiya na Kikatiba  Chama Cha Mapinduzi baada ya kukidhi masharti ya Kikanuni na Kikatiba bila kukiuka hatua husika .
 
Aidha tunasisitiza hatutamvumilia mtu au kikundi cha watu wenye dhamira ya kuichafua Jumuiya ya Umoja wa Vijana na Chama kwa kisingizio cha Uchaguzi. Chama chetu inaheshimika kwa demokrasia iliyotukuka Afrika na Duniani kwa ujumla hivyo sisi Vijana lazima tusimame imara kulinda heshima hiyo.

Mwisho Umoja wa Vijana wa CCM unaendelea kuwapongeza Vijana wote nchini kwa kuendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Joseph Magufuli , kwa kazi nzuri ya kizalendo ya  kuiletea Tanzania mabadiliko ya kimfumo na Kiutawala, Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa.

Wote tuna wajibu usioepukika kila mmoja kwa nafasi yake,  tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu amzidishie  afya njema, ampe umri mrefu, moyo wa ujasiri na uthubutu katika kupanga na kutekeleza majukumu ya Kiserikali na ya Kisiasa.
 
Nawatakia kila la heri.
 
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
 
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com