Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera
Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera
amewaonya wakazi wa mkoa huo kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa na kuendesha
vitendo vya ujangili kwani wakibainika Serikali itawachukulia hatua
kali za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari
juzi baada ya kufunga tamasha la kupinga ujangili lililoandaliwa na
Taasisi ya Chemchem Foundation katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya
Burunge, Bendera alisema wote waliovamia maeneo ya hifadhi wataondolewa.
“Kuna
familia kama 17 zinaishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Jamii Burunge,
tayari wamepatiwa eneo la kwenda na tunaonya ambao watavamia maeneo ya
hifadhi na kufanya ujangili kuwa watachukulia hatua kali za kisheria,”
alisema.
Awali, akitoa taarifa ya utendaji, Mkurugenzi
wa Chemchem Foundation, Nicolaus Negri aliwataka wananchi wanaoishi
vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Jamii Burunge kukataa ujangili.
Negri
alisema wananchi wanapaswa kukataa kununua nyama za porini kutoka kwa
majangili, lakini pia wanatakiwa kutoa taarifa polisi kwa watu
wanaojihusisha na biashara hiyo mitaani.
“Kama tukiacha
ujangili uendelee na tukaendelea kuvamia maeneo ya hifadhi, ina maana
tutakosa watalii hivyo shughuli za maendeleo zitakwama,” alisema Negri.
Taasisi
ya Chemchem imewekeza kwenye hoteli katika eneo la Burunge na inamiliki
kitalu cha uwindaji. Eneo hilo linapakana na hifadhi za Tarangire na
Manyara ambazo hutembelewa na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.
0 comments:
Post a Comment