METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 26, 2017

KATIBU MKUU KITILA AZINDUA JUKWAA LA WADAU WA MAJI ARUSHA

Katibu Mkuu wa Wizara  ya Maji na Umwagiliaji , Profesa Kitila Mkumbo,Akizindua Jukwaa la wadau kuhusu usimamizi na utunzani wa maji katika Bonde la Pangani jijini Arusha juzi(Habari Picha na Pamela Mollel Arusha)
Mwenyekiti wa Jukwaa Jukwaa la wadau kuhusu usimamizi na utunzani wa maji
katika Bonde la Pangani
 Mhandisi Mbogo
Futakamba, alisema pamoja na vyanzo vingi vya maji vilivyopo nchini, lakini
kuna changamoto katika matumizi kwa maendeleo ya kiuchumi.

Mhandisi wa Maji Mkoa wa Arusha, Joseph Makaidi,
alisema, baadhi ya maeneo hali ya upatikanaji wa maji ni nzuri ikilinganishwa
na maeneo mengine.
 Afisa Maji kutoka Bonde la Pangani, Mtoi Kanyawanah,akizungumza na vyombo vya habari 
Baadhi
ya washiriki wakiwa katika picha ya pamoja
…………………………………………………………………….
Na Pamela Mollel,Arusha
 
WIZARA ya Maji na Umwagiliaji, imeweka mkazo katika utunzaji
wa maeneo ya vyanzo vya maji huku ikitaka wadau wa maji kushirikishwa
kikamilifu katika mipango ya uanzishwaji wa viwanda.

 
Aidha imetaka sekta binafsi kushirikishwa katika usimamizi wa
raslimali maji kwa kutoa elimu kwa wananchi kutovamia vyanzo vya maji huku
ikiwataka waliovamia watoke.

 
Akizindua Jukwaa la wadau kuhusu usimamizi na utunzani wa
maji katika Bonde la Pangani jijini hapa jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Profesa Kitila Mkumbo, alisema, maji ni injini ya uchumi.

 
 “Maji yanachangia ukuaji wa kila sekta, bila maji kwa
mfano, hakuna viwanda, kilimo, ufugaji wala huduma zingine za kijamii.

 “Maji ni injini ya uchumi, lakini kwa bahati mbaya maji
yamepungua wakati matumizi yake yakiongezeka kila siku,” alisema.

Akizungumzia hali ya maji nchini, alisema ina sura mbili,
moja ni nchi yenye vyanzo vingi vya maji, wakati sura ya pili ni nchi
inayokabiliwa na uhaba wa maji.

 
“Upungufu huu unatufanya kuona ulazima wa kutunza vyanzo vya
maji vilivyopo kwa kushirikisha wadau na kutoa elimu kwa wananchi ili
wasiendelee kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji,” alisema na kuongeza,
“waliovamia vyanzo hiyo watoke.”

 
 Alisema kutokana na ongezeko la changamoto kuhusu
usimamizi wa raslimali maji, anaamini sekta binafsi ambayo inategemea na
kunufaika na matumizi ya maji ina jukumu kubwa la kufanya katika kutunza na
kuhifadhi vyanzo vya maji.

 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Mhandisi Mbogo
Futakamba, alisema pamoja na vyanzo vingi vya maji vilivyopo nchini, lakini
kuna changamoto katika matumizi kwa maendeleo ya kiuchumi.

 
Alisema kwa mfano, katika suala la uanzishaji wa miradi na
viwanda ni lazima kupanga kwa pamoja wakianzia na suala la maji.

“Tukianza na maji tutapata viwanda, mifugo, kilimo na huduma
za kijamii,” alisema.

 
Akizungumzia hali ya maji mkoani Arusha, Mhandisi wa Maji
Mkoa, Joseph Makaidi, alisema, baadhi ya maeneo hali ya upatikanaji wa maji ni
nzuri ikilinganishwa na maeneo mengine.

 
Alisema maeneo ya vijijini yanapata maji safi kwa asilimia
60.25 ingawa hayajatibiwa wakati maeneo ya mijini yanapata kwa asilimia 40.

 
Hata hivyo, alisema kuna tatizo la upatikanaji wa maji safi
na kwa baadhi ya maeneo hususan, Arumeru kutokana na wingi wa madini ya 
Fluoride katika maji.
Afisa Maji kutoka Bonde la Pangani, Mtoi Kanyawanah, alisema,
inategemea na mvua inavyonyesha kwa mwaka.

 
Alisema kama kuna mvua nzuri kwa mwaka upatikanaji wa maji
katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na Hale na maeneo mengine unakuwa mzuri.

Kwa ujumla, “hali ya maji siyo nzuri wala siyo mbaya, na hii
inategemeana na unyeshaji wa mvua.”

 
Pamoja na wadau wengine, uzinduzi wa jukwaa hilo
ulishirikisha wawakilishi kutoka taasisi za International Water Stewardship
Programme (IWaSP), Ukaid na GIZ.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com