Dar es Salaam. Kampuni ya Quality Group (QGL)
limited inayomilikiwa na Yusufu Manji imelaani utaratibu uliotumiwa na
kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart kufunga ofisi zake, hivyo
inakusudia kuchukua hatua za kisheria.
Ofisi hizo
zilizopo jengo la Quality Plaza zilifungwa siku tatu zilizopita kwa
madai kuwa inadaiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), Sh12.2 bilioni.
Mshauri
Mkuu wa masuala ya sheria wa QGL, Stefano Alderighi alisema jana kuwa
haamini kama kamishna wa TRA anahusika katika tukio hilo.
“Yono walipokuja tuliwaomba vitambulisho, lakini walitujibu kuwa hawana na hakuna haja ya kutupa,” alisema Alderighi.
“Hata
tulipowaomba kibali cha TRA walituonyesha nyaraka ambazo hazijatiwa
saini na kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, jambo ambalo linatuaminisha kuwa
huenda kamishna hafahamu chochote kuhusu watu hao.”
Alisema
QGL inalaani utaratibu uliotumiwa na Yono kwanza kwa kutoonyesha
vitambulisho na nyaraka zinazowapa mamlaka na pia kwa kutowapa muda
wafanyakazi kuondoka ofisini na vitu vyao binafsi.
“Yono
walitumia kama dakika tano tu, waliwalazimisha watumishi wote kutoka
nje ya ofisi bila kuwapa muda wa kuchukua vitu vyao. Lakini pia
hawakuwaheshimu wageni wa ndani na nje waliokuwa katika kituo cha afya
cha kampuni ambacho nacho walikifunga,” alisema Alderighi.
Alisema
tayari uongozi wa kampuni umeomba kuonana na kamishina mkuu wa TRA ili
kumtaarifu suala hilo na kuomba ushauri wa namna ya kufanya kabla ya
kufungua shauri dhidi ya Yono.
Pia alimuomba kamishna
huyo kukifungulia kituo cha afya cha kampuni hiyo kwa kuwa hakihusiki na
madai hayo ya kodi, lakini pia kwa ajili ya ustawi wa umma.
Hata
hivyo, siku ambayo ofisi hizo zinafungwa, mkurugenzi wa huduma na elimu
kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema wamekuwa na mawasiliano
na kampuni ya Farm Equipment ambayo inamilikiwa na Manji tangu Agosti
15, lakini kulikuwa hakuna mrejesho kuhusu deni hilo.
Lakini
Alderighi alisema wamewasiliana na TRA kuhusu madai yao mara mbili
kabla ya tukio hilo na hata baada ya kufungiwa ofisi, wamewaandikia
barua na wataendelea kushirikiana nao.
Akijibu madai hayo, mkurugenzi wa Yono, Consolata Yono alisema wanaongozwa na utaratibu kutoka TRA.
“Ni
vigumu kwenda kufunga ofisi ya mtu bila kuwa na nyaraka zote muhimu.
Hao kama wanadaiwa walipe tu sio kuanza kusingizia eti wameonewa,”
alisema Yono.
0 comments:
Post a Comment