NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo amefanya ziara leo ya kukagua
utekeleza wa maagizo ya serikali aliyoyatoa hivi karibuni katika Kituo cha Afya
Makole Manispaa ya Dodoma.
Pamoja na maagizo mengine, Jafo aliagiza
kuhakikisha kituo hicho kinafunga mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato.
Akiwa katika ziara yake leo, Jafo amepongeza
ufungaji wa mfumo huo huku akiwataka kuhakikisha wanaziba mianya ya upotevu wa
mapato kwa kuwa hali ya ukusanyaji bado hairidhishi.
Amesema kwa mujibu wa taarifa aliyoipata kituo
hicho kabla ya mfumo kilikuwa kikikusanya Sh.Milioni nne lakini kwasasa
kinakusanya hadi Sh.Milioni 9.9 kwa mwezi jambo ambalo linaonesha bado kuna
mianya ya upotevu wa mapato.
“Nawapongeza kwa kutekeleza maagizo ya serikali kwa
kufunga huu mfumo lakini sijaridhishwa na ukusanyaji mapato wa kiwango hichi,
kuna vituo vinakusanya hadi Sh.Milioni 24 nyie mnakusanya hivi bado haitoshi
hakikisheni mnaziba mianya,”amesema Jafo
Ameongeza “Kuwepo
na mfumo ni jambo moja na kuutumia mfumo ni jambo jingine jambo la msingi ni
uaminifu kuna watu katika vituo vyetu uaminifu ni mdogo kwenye kukusanya fedha
ndio ugomvi huwa unazuka na wakati mwingine watu wanatolewa kwa maslahi yao
binafsi,”.
Amewataka kuhakikisha kunakuwepo na matumizi sahihi
ya mfumo huo ili kuongeza mapato.
Akizungumzia kuhusu ujenzi na ukarabati wa vituo
vya afya nchini, Jafo amesisitiza Mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha
zinasimamia kikamilifu ujenzi huo na ifikapo Desemba 30 mwaka huu uwe
umekamilika.
Amesema hivi karibuni serikali imetoa Sh.Milioni
500 kwa kila kituo kimoja kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo
jengo la upasuaji,maabara ya kisasa na wodi ya akina mama na watoto.
Naibu Waziri huyo amesema serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Dk.John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya na kwamba
utoaji wa fedha huo umetokana na hali ya vituo vya afya kuwa si ya kuridhisha.
Amebainisha Dodoma ni eneo mkakati kutokana na
wingi wa watu hivyo ni lazima huduma za
afya ziboreshwe ili kuondoa msongamano katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa
Dodoma.
Kwa upande wake, Katibu wa Afya wa kituo hicho, Habiba
Thabiti amesema kabla ya kufungwa mfumo huo walikuwa wanakusanya Sh.Milioni nne
kwa mwezi lakini kwasasa wamefikia Sh.Milioni 9.9.
Naye, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk.George
Matiko amesema kwa siku kituo kinahudumia wagonjwa kati ya 400-800 na akina
mama wanaojifungua kwa mwezi ni 400.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi
Selemani Jafo akisisitiza jambo alipokuwa akikagua mfumo wa kielektroniki
katika Kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma.Wagonjwa wakiwa katika dirisha la malipo kwenye kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma
Wagonjwa wakiwa katika dirisha la malipo kwenye kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akisalimia wagonjwa alipokuwa akikagua kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi
Selemani Jafo akisisitiza jambo alipokuwa akikagua mfumo wa kielektroniki
katika Kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma.
0 comments:
Post a Comment