METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 16, 2017

TUNAJIVUNIA KUPIGA VITA ADUI NJAA: DKT MWANJELWA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akisisitiza Jambo Wakati akitoa salamu katika kilele Cha Maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Katika Viwanja vya CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza jambo mbele ya Meneja uwezeshaji wakulima wadogo katika Benki ya Wakulima Tanzania (TADB) Ndg Daniel Mabula, Mwingine ni Naibu waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa Mara  Baada ya kutembelea banda la  Benki hiyo Wakati wa maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo Kitaifa yalifanyika Katika Viwanja vya CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akizungumza na wananchi Wakati akitoa salamu katika kilele Cha Maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yalifanyika Katika Viwanja vya CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa (Kushoto), Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na watumishi mbalimbali wa umma wakitembelea mabanda mbalimbali katika kilele Cha Maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yalifanyika Katika Viwanja vya CCM Kalangalala Mkoani Geita.

Na Mathias Canal, Geita

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa amesema kuwa serikali inatekeleza kwa vitendo kupigaja vita adui njaa, umaskini na maradhi.  

Alisema katika kupiga Vita adui njaa tayari uzalishaji umeongezeka katika mazao makuu ya chakula hususani mahindi, mchele, mtama, uwele, na mikunde.  

Aliyataja mazao mengine ambayo uzalishaji wake umeongezeka kuwa Ni pamoja na uzalishaji wa mazao ya jamii ya mizizi kama muhogo, ndizi, viazi vitamu na mviringo.

Mhe Dkt Mwanjelwa ameyasema hayo Wakati akitoa salamu katika kilele Cha Maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Katika Viwanja vya CCM Kalangalala Mkoani Geita.

Alisema kuongezeka kwa uzalishaji katika mazao hayo kumepelekea Taifa kujitosheleza kuwa na chakula kwa wastani wa zaidi ya asilimia 100. 

Alisema Mwaka 2016 Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2015 ambapo Mchango mkubwa katika Pato la Taifa ulitokana na Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine za kiuchumi.

Dkt Mwanjelwa Alisema Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula mwaka huu isemayo “Badili mwelekeo wa uhamaji; Wekeza katika usalama wa chakula na maendeleo Vijijini” inaweka umuhimu katika kuweka Mipango na Programu zinazolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo Vijijini; kupunguza utegemezi na kuongeza usawa katika Jamii.

Alisema Sambamba na hayo pia inaakisi na kutilia msisitizo uhifadhi mazingira ambayo ndiyo muhimu katika maendeleo ya kilimo na hifadhi ya Jamii ili kuchochea jitihada za kuondoa umaskini kwa kutumia nguvukazi ya Rasilimali Watu hususani  Vijana ambayo imekuwa ikihamia Mijini kwa lengo la kujitafutia mahitaji ya muhimu na mazingira bora.

Katika hatua nyingine Mhe Naibu Waziri alitembelea na kujionea juhudi zilizofanywa na Wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa Taifa linajitosheleza kwa chakula, kujipatia bidhaa za viwandani na pia kupata mazao ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi ili kumpatia Mkulima na Mfugaji faida.

Maadhimisho hayo yalifungwa rasmi jana Octoba 16, 2017 na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ambapo alisisitiza kuwa mafanikio yanayopatikana katika sekta ya Kilimo nchini Ni kutokana na juhudi na umahiri na uwajibikaji unaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli yaliyopelekea Nchi kujitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100.

Aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita kwa maandalizi mazuri na kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu wa 2017.

Pia aliwashukuru Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Kilimo kwa ushirikiano wao kufanilisha Maadhimisho hayo ikiwa Ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Mpango wa Chakula (WFP - World Food Program) sambamba na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO - Food and Agriculture Orgization)

Maadhimisho ya kwanza ya siku ya chakula Duniani yalianza mwaka 1981. Hivyo maadhimisho ya mwaka huu ni ya 36 na yanasherehekewa kwa pamoja na maadhimisho ya  miaka 72 ya kuanzishwa kwa FAO tarehe 16 Oktoba, 1945.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com