Obadia Frank alipofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
MKAZI wa Chato mkoani Geita,
Obadia Frank (41), mapema leo amefikishwa katika mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo kupitia
mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu mazungumzo kati ya Serikali na
wawakilishi wa kampuni ya Acacia.
Akisomewa hati ya mashtaka na
wakili wa serikali, Leonard Challo, amedai mshtakiwa huyo ambaye ni
wakala wa Bayport ametenda kosa hilo Agosti 8 mwaka huu, katika Wilaya
ya Chato mkoani Geita.
Imedaiwa mbele ya Hakimu
Mkazi, Wilbard Mashauri, kuwa siku hiyo mshtakiwa alichapisha taarifa
kupitia ukurasa wake wa Facebook uliokuwa ukihusiana na mazungumzo kati
ya serikali na kampuni ya Acacia.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza
maneno kuwa “Taarifa kutoka kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na
wawakilishi wa kampuni ya Acacia kuwa wanasheria wa upande wetu
wanashindwa kutafsiri baadhi ya vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba
msaada kwa wanasheria wa Acacia sasa huoni hivi ni vituko mwizi
anakusaidia sheria haahaa haha.”
Inadaiwa aliendelea kusambaza
maneno kuwa, “mazungumzo bado yanaendelea lakini wanasheria wetu
wamebanwa sana ukizingatia wale jamaa wana vielelezo vyote vya mikataba
kiukweli tumuombe Mungu maana Serikali ikitaka kuvunja mkataba na Acacia
gharama kubwa zitatuusu.”
“Lakini pia kuendeleza uvyama
utatugharimu saana, baada ya mh. Rais Magufuli angewashirikisha mawakili
wasomi waliokwishaiva wakili Lissu, wakili Kibatara na Fatma Karume
kwenye mambo ya umuhimu kama haya yeye kaleta uchama sasa itatugharimu
.// Dicteta Magufuli mist go”.
Maneno hayo yanadaiwa kusambazwa na
mshtakiwa huyo kupitia mtandao huo wa kijamii wa Facebook.
Imedaiwa mshitakiwa ametenda hayo huku akijua kuwa taarifa hizo ni uongo na zilikuwa na nia ya kuipotosha jamii.
Hata hivyo mshtakiwa huyo
anayetetewa na wakili Peter Kibatala, amekana kutenda kosa hilo na
amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti na kesi hiyo
itatajwa Oktoba 16 mwaka huu.
Mahakama imemtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao walitakiwa kuweka bondi ya Sh. milioni tano.
NA DENIS MTIMA/GPL
0 comments:
Post a Comment