Serikali
kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kutoa
hati mpya za ardhi zenye umri wa miaka 99 tofauti na zile zilizokuwa
zikitolewa awali za miaka 33.
Akizungumza
na wanahabari jana Mjini Dodoma Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi amesema zoezi hilo la ubadilishaji wa hati kwa
wakazi elfu 25 wa mkoa huo limeanza rasmi ambapo wakazi hao wanatakiwa
kufika Wizarani wakiwa na nakala za hati zao za zamani ambazo zimelipiwa
kodi zote za ardhi.
“Ubadilishaji
wa hati hizi ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli
alipoivunja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ambapo aliiagiza
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kubadilisha hati
zilizokuwa zikitolewa na mamlaka hiyo kutoka umiliki wa miaka 33 na kuwa
miaka 99,” alifafanua Lukuvi.
Aliongeza
kuwa hati hizo za miaka 33 zilikuwa zikiwanyima fursa wakazi wa Dodoma
kupata wawekezaji kutoka nje ya nchi kutokana na hati hizo kuwa za muda
mfupi tofauti na hati zinazotolewa na miji mingine hapa nchini.
Aidha
hati hizo pia zilikuwa kikwazo kwa wamiliki kushindwa kupata mikopo
mikubwa ambayo hutolewa kwa watu wenye umiliki wa ardhi wa kuanzia miaka
50 na kuendelea.
Lukuvi
amesema kuwa mabadiliko hayo ya hati hayata athiri mipaka ya viwanja
vitakavyobadilishiwa hati bali kinachofanyika ni kubadilisha umri wa
umiliki wa ardhi.
0 comments:
Post a Comment