Na Mathias Canal, WEST-Kigoma
Serikali
kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ina mpango
wa kuanzisha kampasi ya MUHAS mkoani Kigoma.
Kampasi
hii itajengwa katika Halmashauri ya Ujiji mkoani Kigoma katika eneo la ekari
47.3 ambalo linapakana na eneo litalojengwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya
Magharibi.
Kampasi
hii inatarajiwa kuwa na miundombinu itakayotoa mazingira bora ya ufundishaji na
kujifunzia, utafiti pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 17
Octoba 2022 Wilayani Kasulu wakati wa ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan Mkoani Kigoma.
Waziri
Mkenda amesema kuwa serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia imetenga kiasi cha
dola za Marekani milioni 45.5 kwa ajili ya MUHAS. Kati ya fedha hizo, kiasi cha
dola za Marekani milioni 15 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika
kampasi ya Kigoma.
Kadhalika,
Waziri Mkenda amemshukuru Rais Samia kwa kuzindua majengo mapya ya Chuo cha
Ualimu Kabanga ambayo ni moja kati ya Miradi iliyotekelezwa na Wizara ikiwa ni
Mkakati wa Serikali wa kuboresha Mazingira ya utoaji wa Elimu ya Ualimu nchini.
Prof Mkenda amesema kuwa Ujenzi
huo umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya
Ualimu nchini (Teachers Education Supports Project – TESP).
Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga ulianza
tarehe 26/03/2019 na ulikamilika tarehe 22/04/2022. Ujenzi
umetekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT Kanda ya Magharibi chini ya Usimamizi wa
Mshauri Elekezi Bureau for Industrial Cooperation (BICO) wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam. Aidha, kazi ya utengenezaji na uwekaji wa Samani katika majengo haya
inaendelea.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa Mradi huo umegharimu
jumla ya Shillingi za Kitanzania 14,142,554,960.53 ambapo Sh. 12,591,407,901.26
ni kwa ajili ya ujenzi wa majengo na Sh. 1,551,147,059.27 ni kwa ajili
ya utengenezaji na uwekaji wa Samani na utakuwa na uwezo wa wa kuchukua wanachuo
800.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment