Aliyekuwa Mkurugenzi wa Masuala ya
Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof.
Hermas Mwansoko akitoa mada kuhusu masula ya utamaduni mbele ya Wajumbe
mbalimbali waliohudhuria mkutano unaohusiana na masuala ya Tamasha la
Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) mjini Kampala, Uganda 12
Septemba, 2017.
Baadhi ya Washiriki wa mkutano
uliohusisha utoaji mada wa baadhi ya Viongozi mbalimbali toka nchi
wanachama pamoja na wageni waalikwa kuhusiana na masuala ya umuhimu wa
Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) wakisikiliza
uwasilishaji mada ukioendelea mjini Kampala, Uganda leo 12 Septemba,
2017.
………………………..
Na Benedict Liwenga-WHUSM, Kampala
Watanzania wametakiwa kuuenzi na
kuulinda utamaduni wao kupitia Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika
Mashariki (JAMAFEST) ili waweze kuleta maendeleo katika masuala ya
ujasiriamali, utalii na pia kuufanya uwe bidhaa yao katika kuutambulisha
utanzania wao hususani katika masuala ya vyakula, mavazi ya asili,
nyumba za asili, utamaduni usioshikika pamoja na lugha ya Kiswahili.
Kauli hiyo imetolewa leo Mjini
Kampala, Uganda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo, Prof. Elisante Ole-Gabriel katika Tamasha la Kiutamaduni na
Sanaa kwa nchi za Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST.
Prof. Elisante ameeleza kuwa,
Utamaduni ndiyo silaha pekee inayoweza kuwaweka watu pamoja ambapo
amesisitiza kuwa, Watanzania hawanabudi kuulinda utamaduni wao ili uweze
kuwaletea maendeleo huku akigusia suala la lugha ya Kiswahili, matumizi
ya vyakula vya asili, matumizi ya mavazi ya asili pamoja na nyumba za
asili kuwa vitu hivyo vina uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo nchini.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya
lugha ya Kiswahili alisema kwamba, lugha hiyo imekuwa ni ya 10 kati ya
lugha zinazozungumzwa Duniani na inazungumzwa na watu zaidi ya nchi 50
katika Bara la Afrika.
Ameongeza kuwa, lugha ya Kiswahili
inaweza kutumika kama bidhaa ambapo juhudi za kutosha kupitia Wizara
yake zinafanywa katika kuhakikisha kuwa lugha hiyo inatumika zaidi kwa
ufasaha na kubidhaishwa ulimwenguni kote.
“Kupitia Baraza la Kiswahili la
Taifa (BAKITA), tunahakikisha kwamba Kiswahili kinabidhaishwa ndiyo
maana hivi karibuni Waziri wetu Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
alizindua Kamusi Kuu ya Kiswahili Bungeni Mjini Dodoma, kwahiyo tukio
lile limekuwa chachu ya pekee na limeongeza uzito mkubwa katika lugha ya
Kiswahili”, alisema Prof. Elisante.
Amebainisha kuwa, Tamasha la
JAMAFEST litasaidia kuondosha tofauti mbalimbali baina ya nchi za Afrika
Mashariki na litasaidia kuzifanya nchi hizo kuwa kitu kimoja kwakuwa
zitakuwa zinashikamana na lugha ya Kiswahili ambayo kwa kiasi kikubwa
inatumika katika nchi hizo.
“Tukiweka utamaduni wetu ukawa
unaingiliana basi tutafika muda itabidi tuanze kusahihisha zaidi
kufafana kwetu na sio kutofautiana kwetu na hakika hakuna
atakayebaguliwa kwani umoja wetu huo utaleta faida kubwa katika masuala
ya uchumi wa viwanda kwasababu soko litakuwa kubwa baina ya nchi zetu za
Afrika Mashariki”, alisema Prof. Elisante.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Bodi ya Filamu, Bibi Joyce Fissoo amesema kwamba, Tamasha la JAMAFEST
limeleta fursa mbalimbali katika masuala ya utamaduni kama vile vivutio
vya kiutamaduni, vivutio vya kiasili, ambapo Tanzania imepata fursa ya
kuwa na mada tano zinazozungumzia masuala ya hifadhi, masuala ya filamu
hususani mchango wa filamu katika uchumi wa Taifa, masuala ya filamu na
muziki, masuala ya Sheria na taratibu zinazosimamia sekta za utamaduni
na ubunifu.
Amefafanua kuwa, mada ambazo
zimetolewa na Viongozi mbalimbali toka Tanzania zimeakisi masuala muhimu
ya utamaduni, umuhimu wa kuuhifadhi utamaduni, umuhimu wa sekta za
ubunifu zikiwemo na filamu.
“Tamasha la JAMAFEST linasaidia
kuimarisha utangamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, linatanua wigo wa masoko ambapo bidhaa mbalimbali
zinapatikana toka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, pia linatangaza
vivutio vya nchi wanachama, lakini pia linatangaza rasilimali za nchi
wanachama ambapo kwa upande wa Tanzania tumeweka mambo ya kipekee jambo
ambalo limewavutia watu mbalimbali kuja kuona vitu vyetu”, alisema Bibi
Fissoo.
Katika Tamasha hilo, Tanzania
imewakilishwa na wadau wapatao 247 ambapo kati yao 71 wanatoka Tanzania
Visiwani (Zanzibar) ambapo baadhi ya vikundi vya ngoma na bendi
vimehudhuria pia kwa upande wa Tanzania Bara kuna vikundi mbalimbali vya
Sanaa toka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBA) pamoja na vinginevyo
ambavyo vimehudhuria katika Tamasha hilo.
“JAMAFEST ni fursa kwa nchi
wanachama kwakuwa nje ya utamaduni, ubunifu, na mitindo tamasha hili
linatoa fursa ya mapato kwahiyo kwa kiasi kikubwa tumechangia kwa namna
moja au nyingine kuongezeka kwa mapato kwa moja ya nchi wanachama ambayo
ni Uganda, lakini tunatarajia na sisi kwa tamasha lijalo kufanyika
kwetu hapo baadaye itakapotangazwa”, aliongeza Bibi. Fissoo.
Kaulimbiu katika Tamasha hilo
ambalo lilianza mwaka 2013 nchini Rwanda linasema ‘Utamaduni na Ubunifu,
Kiini cha Ajira na Umoja’. Tamasha hilo linahusisha mambo mengi baina
ya nchi wanachama hususani masuala ya vivutio vya utamaduni wa asili.
0 comments:
Post a Comment