METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 13, 2021

ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 24.7 KUTUMIKA KUVIPELEKEA UMEME VIJIJI 53 VILIVYOSALIA MKOANI KATAVI

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akizungumza na wanakijiji wa Katambike (Hawamo pichani) tarehe 12 Julai, 2021, alipotembelea kijiji hicho kilichopo katika Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.

 

Wanakijiji cha kijiji Katambike, Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi wakimsikiliza Naibu Waziri Byabato (Hayumo pichani) alipokuwa akizungumza nao kufuatia ziara yake ya kikazi kijijini hapo

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda (Mb.) akizungumza na wanakijiji wa Katambike (Hawamo pichani) tarehe 12 Julai, 2021, alipoungana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Byabato katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Katambike, kilichopo katika Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi.

 

Picha zinazoonyesha eneo la Ugalla.

Na Dorina Makaya – Katavi

Serikali itatumia zaidi ya shilingi bilioni 24.7 kuunganisha umeme kwenye vijiji 53 ambavyo bado havijaunganishiwa umeme mkoani Katavi katika Mradi Kabambe wa kupeleka umeme vijijini Awamu ya III Mzunguko wa pili.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato tarehe 12 Julai, 2021, alipotembelea kijiji cha Katambike, Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi akiwa katika  ziara ya kikazi mkoani humo.

Amesema, Serikali inatambua, umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoani Katavi na kuwa MW 5.3 zinazozalishwa katika kituo cha Mpanda bado hazitoshelezi mahitaji ya umeme hususan katika kuwezesha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya viwanda na biashara hapa nchini.

Naibu Waziri Byabato ameeleza kuwa, Serikali imeamua kuleta grid ya Taifa mkoani Katavi ili kuwa na umeme wa uhakika mkoani humo na tayari ujenzi wa majengo ya vituo vya umeme kuleta grid ya Taifa mkoani Katavi umefikia zaidi ya asilimia 90.

Amevitaja vituo hivyo kuwa ni Ipole, Inyonga na Mpanda.

Ameongeza kuwa, pesa kwa ajili ya kuleta umeme mkoani Katavi ipo, na zitawekwa Transfomer mbili zenye ukubwa wa 15MVA kila moja sawa na 12MW, zitakazowekwa kwenye kituo cha Inyonga na nyingine katika kituo cha Ipole ili kuhakikisha kila kituo kinatoa umeme wa kutosha na wa uhakika.

Naibu Waziri Byabato amesema, mradi wa Grid ya Taifa kwa mkoa wa Katavi utakamilika ifikapo Agosti, 2023.

Amewaeleza wananchi wa kijiji cha Katambike kuwa, umeme utakuwa umefika kijijini hapo ifikapo mwezi Octoba mwaka 2021, na kuwa hakuna kijiji kitakachoachwa kuunganishiwa umeme.

Amewaasa wanakijiji cha Katambike kuanza kufanya maandalizi ya kupokea umeme kwa kuanza kutandaza nyaya kwenye nyumba zao (Wiring) na kulipia shilingi elfu 27,000 tu ili waweze kuunganishiwa umeme utakapofika kijijini hapo.

Aidha, amewaomba wanakijiji hao kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuhakikisha miundo mbinu inatunzwa na kutoharibiwa kwa nguzo na kuonya kuwa atakayebainika kuiharibu miundombinu ya umeme atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mbunge wa jimbo la Nsimbo, Mhe. Anna Lupembe amemshukuru Naibu Waziri Byabato kwa kufika mkoani Katavi, kujionea hali halisi ya umeme mkoani humo na kutoa ahadi ya kuvipelekea umeme vijiji 53 ambavyo bado havijaunganishwa umeme na kuahidi kufikisha umeme kijijini Katambike ifikapo mwezi Octoba 2021.

Mhe. Lupembe, amesema, kupatikana kwa umeme katika kata ya Ugalla kutasaidia sana katika kuinua kilimo cha mpunga na kuwezesha mazingira ya uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo vitakavyoboresha bidhaa ya mchele katika viwango vya juu zaidi na kuwaongezea kipato wananchi wa Ugalla.

Awali Naibu Waziri Byabato alitembelea vituo vipya vinavyojengwa vya Ipole, Inyonga na Mpanda na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa vituo hivyo.

Mara baada ya kuwasili katika wilaya ya Mlele tarehe 11 Julai, 2021 Naibu Waziri Byabato alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filiberto Sanga na kupata taarifa kuhusu upatikanaji wa umeme Wilayani Mlele.

Aidha tarehe 12 Julai, 2021 kabla ya kuanza ziara yake katika kata ya Ugalla mkoani Katavi, Naibu Waziri Byabato alikutana na Mkuu wa mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko na kupata taarifa ya upatikanaji wa umeme kwa mkoa wa Katavi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com