METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 10, 2017

UVCCM YALAANI MATAMSHI YA BAVICHA KWA KUKOSA STAHA

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umelaani vikali Matamshi ya Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) yenye nia na lengo la kupalilia chuki kwa kuthubutu kuingilia medani za kintelejinsia na upelelezi kufuatia tukio la kusikitisha la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki Mheshimiwa Tundu Antipius Lissu na watu wasiojulikana.

UVCCM imesema Septemba 9 Mwaka huu Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) kupitia Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake walikutana na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kutoa matamshi ya kebehi, yanayojenga utata na mkanganyiko katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 10, 2017 na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya makao makuu ya UVCCM Jijini Dar es salaam.

Alisema Fikra na mtazamo wa BAVICHA licha ya kutakiwa kulaaniwa vikali na kila mwananchi pia una nia potofu ya kutaka kuiyumbisha jamii hivyo hawapaswi kupewa nafasi badala yake kupuuzwa na watanzania wote werevu, wapenda amani, umoja na mshikamano.

Shaka alisema kuwa Tukio la kushambuliwa Mheshimiwa Tundu Lissu na watu wasiojulikana si jambo dogo na jepesi kama inavyochukuliwa na BAVICHA na viongozi wake ambao wameshindwa kupima uzito wa maneno yao kabla ya kutamka kwani Yapo matukio mengi ya kijambazi huko nyuma yamewahi kutokea Mengine yamepoteza maisha ya viongozi wa juu wa Serikali na kukatisha maisha yao kabla ya tukio la Mheshimiwa Lissu lakini BAVICHA hawajawahi kusema.

Alisema lipo tukio la kupigwa risasi nane kifuani Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, kuuawa kwa aliyekuwa Waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Nickas Mahinda Mkoani Morogoro kwa tukio la kupigwa risasi.

Alisema nchini Marekani Marais wawili katika familia moja ya kina F. Kennedy waliuawa katika mazingira ya kihalifu lakini pia Rais Anuar Saadat wa Misri aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa anakagua gwaride.

Alisema UVCCM ilitegemea kuona ujasiri wa BAVICHA kujigamba na kuwapa kiburi cha kuhoji, wangehoji mazingira tata ya kifo cha Profesa Kighoma Ali Malima Uingereza au kifo cha Kapteni Ditopile Ukiwaona Mzuzuri Mkoani Morogoro .

Aliongeza kuwa yapo Matukio ya ujambazi yanayofanywa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi watu mbalimbali ni mambo yanayotokea hata katika Mataifa makubwa na baadhi ya matukio mara nyingi upelelezi wake huchukua miaka na muda mrefu hadi wahusika kutambuliwa au kukamatwa.

Umoja wa Vijana wa CCM unawakanya Bavicha nakuwataka waache kiherehere cha kuingilia taratibu za kiutawala na upelekezi, yanapotokea masuala mazito yakihusisha maisha ya watu, kushambuliwa au kutekwa na wao kutaka kuyageuza yaonekane katika muktadha wa kisiasa.

Shaka alisema kuwa BAVICHA wamejitahidi kuanisha matukio kadhaa walioyaita yamefanywa na watu wasiojulikana, upelelezi wake kutojulikana na kutaja baadhi ya majina ya watu waliokumbwa na kadhia ya matukio hayo huku wakikwepa kutaja hata mfululizo wa mauaji ya viongozi wa CCM na Serikali huko Kibiti Mkoani Pwani ambapo pia wamekwepa kutaja kiini cha kifo cha kushangaza cha Marehemu Chacha Zakayo Wangwe.

Aidha, alisema UVCCM kwa mara ya kwanza inaunga mkono matamshi yaliotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Aikael Mbowe aliposema huu si wakati wa kunyooshena vidole vya lawama na shutuma huku akivitaka vyombo vya Usalama vitimize wajibu wao kiufundi na kitaaluma.

Mbowe ametamka matamshi yaliopevuka kifikra, kiupeo na kisiasa tofauti na povu lilivyowatoka vijana wake na kuonyesha uchanga katika siasa huku wakilitumia tukio hili la huzuni la kushambuliwa Mheshimiwa Lissu liwe jukwaa lao la kufanya siasa.

Shaka Aliuliza Kwanini BAVICHA katika maelezo yao hawakugusia wala kuhoji ni kina nani waliomuwekea sumu Dkt Harrison Mwakyembe mpaka akadhurika na kutoka unga mwilini. Je BAVICHA tayari wana majawabu ni nani aliyehusika kumpa sumu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe Wilayani Bagamoyo wakati huo akiwa mwanachama wa CHADEMA.

Hivyo aliwataka viongozi wa Vyama vya siasa kutanguliza mbele maslahi ya umma, kujali na kuendelea kudumisha misingi ya Amani, Umoja wa kitaifa na Mshikamano uliopo.

Alisema UVCCM inaendelea kushauri ni vema kwa wakati huu wananchi kwa ujumla wake wakaongozwa na busara kuliko pupa na ushabiki ambao unaweza kuliingiza taifa katika machafuko yasiyo na msingi na kuharibu tunu ya Taifa ya Amani, Umoja na Mshikamano.

Sambamba na hayo aliongeza kuwa UVCCM inamuombea kwa Mwenyezi Mungu amponyeshe haraka Mhe. Tundu Antiphace Lissu ili aweze kushirikiana na watanzania kujenga na kuliendeleza Taifa.

MWISHO.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com