WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango amesema utapiamlo ni janga la Kitaifa na kwamba theluthi
moja ya vifo nchini inasababishwa na tatizo hilo.
Ametoa kauli hiyo juzi jioni
(Jumatano, Septemba 6, 2017) wakati akitoa nasaha kwenye mkutano wa nne
wa mwaka wa wadau wa lishe wa kutathmini afua za lishe nchini kwenye
ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.
“Haipendezi kuona katika kila
watoto 100, watoto 34 wana udumavu wa akili na katika kila watoto 100,
watoto 59 wenye umri kati ya miezi sita na miaka mitano wana upungufu
mkubwa wa damu,” alisema. Alisema Serikali inatumia asilimia mbili ya
pato la Taifa sawa na dola za Marekani milioni 518 kununua dawa za
vitamin A na folic acid (vidonge vya kuongeza damu).
Alisema kuna haja ya kubuni
mbinu za kilimo ambazo zitainua kiwango cha upatikanaji wa lishe nchini
(nutrition smart agriculture) kama njia ya kudumu ya kukabili tatizo la
utapiamlo na udumavu.
Amesema kwa vile Serikali
imetenga sh. bilioni 11 ili kukabiliana na utapiamlo, wizara yake
itahakikisha inatafuta fedha zilizotengwa na hata ikibidi kutafuta fedha
na misaada ya kitaalamu kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha suala hilo
linatekelezwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Selemani Jaffo aliziagiza
Halmashauri zote nchini zitoe taarifa za kila mwezi za matumizi ya fedha
za afua ya lishe kwenye Kamati zake za Fedha. “Hizi fedha si za kufanya
masikhara, Serikali iko committed katika suala hili,” alisema.
“Zamani katika bajeti za
Halmashauri tulikuwa tukitenga sh. 500 kwa kila mtoto, lakini katika
bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga sh. 1,000 kwa kila mtoto, ambazo ni
sawa na sh. bilioni 11 kwa mwaka,” alisema wakati alipopewa fursa ya
kutoa nasaha zake.
“Wiki iliyopita, Makamu wa Rais alituagiza tuandike performance contracts
kwa Wakuu wote wa Mikoa nchini ili tuweze kufuatilia utekelezaji wao
katika suala zima za kuboresha upatikanaji wa lishe nchini. Kazi hiyo
tumeshaianza na tarehe 22 Septemba, 2017 itakuwa ni siku ya mwisho ya
kukamilisha zoezi hilo,” alisema.
Bw. Jaffo aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya waifanye ajenda ya afya ya lishe kuwa kipaumbele chao.
Wakati huohuo, Naibu Waziri
Jaffo amesema kuwa maafisa lishe 660 wataajiriwa nchini kote hivi
karibuni. Amesema waliopo hivi sasa ni wataalamu 121 tu ambao kati yao
17 wako mikoani na 104 wako kwenye Halmashauri mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa USAID hapa
nchini, Bw. Andrew Karas aliipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa
kuchukua umiliki na usimamizi wa masuala ya lishe ikiwa ni hatua muhimu
ya uratibu wa suala hilo baina ya wahisani, wadau na Serikali.
Alisema ushirikishwaji wa
wadau ni suala muhimu na ambalo haliepukiki lakini akaonya kuwa kuna
haja ya kuangalia namna ya kuongeza uwezo wadau kwa vitendo ili
kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Lengo leni ni letu, na
kipaumbele chenu ni chetu. Tukisaidiana tutaweza kufanikisha suala la
kuongeza lishe na kupunguza atahari za utapiamlo hapa nchini,” alisema
Bw. Karas kwa Kiswahili fasaha na kuamsha shangwe katika ukumbi huo.
Bw. Karas ambaye alizungumza
kwa Kiswahili kwa zaidi ya dakika tano, alikuwa akitoa salamu kutoka
mtandao wa wahisani wa wenye lengo la kufuta utapiamlo kwa kuboresha
lishe nchini (Scaling Up Nutrition -SUN) ambao unajumuisha mashirika ya
Children Investment Fund, DfID, Umoja wa Ulaya (EU), Global Affairs
Canada, Irish Aid na USAID.
Naye Mwakilishi Mkazi wa
UNICEF, Bibi Maniza Zaman, akitoa salamu kwa niaba ya mashirika ya Umoja
wa Mataifa yaliyo chini ya mtandao wa SUN, alisema kufutwa kwa
utapiamlo na kuimarishwa kwa uapikanaji wa lishe bora nchini kunaenda
sambamba na utekelezaji wa malengo 17 endelevu ya maendeleo.
“Kipengele kimojawapo
kikidumaa, kinakwamisha utendaji kazi wa kingine,” alisema na kuongeza:
“Mpango uliozinduliwa unahitaji kuwa na fedha za uhakika ili uweze
kutekelezeka. Inatia moyo kuona Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa
zimetenga bajeti kwa ajili ya mpago huu.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Mtandao wa Masuala ya Lishe Tanzania (Partnership for Nutrition in
Tanzania – PANITA), Bw. Tumaini Mikindo aliiomba Serikali iziwekee uzio
maalum wa kibajeti (ring-fence) fedha za masuala ya lishe ili kuzilinda
zisitumike kinyume na matumizi yaliyopangwa.
“Tunaomba fedha za kasama ya
lishe ziwe ring-fenced ili ziweze kutumika kama zilivyopangwa. Watendaji
watakaofanya vizuri wapongezwe na wale watakaoharibu wachukuliwa hatua
za kinidhamu kwa sababu wanataka kuua Taifa letu,” alisema wakati akitoa
salamu kwa niaba ya mashirika yasiyokuwa ya Serikali zaidi ya 300
yaliyo chini ya mtandao wa SUN.
Alisema mtandao wao umeenea
nchi nzima na akiomba Serikali ilisimamie suala la kupambana na
utapiamlo na kuboresha lishe kwa wananchi wake kama ambavyo ilisimamia
suala la uhaba wa madawati nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
40480 DODOMA,
IJUMAA, SEPTEMBA 8, 2017.
0 comments:
Post a Comment