METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, September 26, 2017

TANAPA YATOA OFA KWA WALIOPO IRINGA KUTEMBELEA HIFADHI YA RUAHA


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (Tanapa) litatumia siku mbili za maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yanayofanyika kwa wiki moja mjini Iringa kutoa usafiri wa gharama nafuu kwa watu wanaotaka kutimiza ndoto zao za kufanya utalii katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa.

Akizungumza na wanahabari jana, meneja masoko wa shirika hilo, Victor Ketansi alisema kwa kupitia maonesho hayo yatakayofanyika kati ya Septemba 27 na Oktoba 2, mwaka huu, Tanapa itafanya safari hizo Septemba 28 na 30.

“Kwa kupitia ofa hiyo kutakuwa na mchango mdogo wa fedha; mtu mzima atalazimika kuchangia Sh 30,000 na mtoto Sh 10,000 tu kumuwezesha kwenda kwa siku moja kutalii katika hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini,” alisema.

Alisema mchango huo unahusisha gharama ya usafiri, kiingilio cha hifadhini, utalii na muongoza wageni atakayewapitisha katika vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo.

“Tuna nafasi 50 tu tumetoa kwa kupitia ofa hii. Safari ya kwanza itahusisha watu 25 na safari ya pili watu 25 pia, kwahiyo wanaotaka wafike na kujiandikisha katika banda letu lililopo katika viwanja vya Kichangani yanapofanyika maonesho haya,” alisema.

Akizungumzia baadhi ya vivutio vilivyoko katika hifadhi hiyo, Mhifadhi wa Idara ya Utalii Ruaha, Hellen Mchaki alisema Hifadhi ya Ruaha pamoja na wingi wa vivutio inabeba pia historia muhimu ya Chifu Mkwawa, kiongozi wa kabila la Wahehe mkoani Iringa aliyeongoza mapambano dhidi ya wajerumani katika karne ya 19.

Alitaja baadhi ya wanyama waliopo katika hifadhi hiyo kuwa ni kudu wakubwa na wadogo, viboko, mamba, pofu, swala pala, makundi makubwa ya samba, tembo na nyati, chui, mbweha, fisi, twiga, pundamilia na mbwa mwitu.

Akizungumzia idadi ya watalii katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Mchaki alisema mwaka 2012/2013 walipokea watalii wa nje 14,299 na wa ndani 9,094, mwaka 2013/2014 wa nje 13,489 na wa ndani 9,673 na mwaka 2014/2015 wa nje 13,272 na wa ndani 8,291.

Alisema mwamko wa watanzania kutembelea vivutio vya utalii bado ni mdogo kwasababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi lakini kwa kupitia maonesho hayo na mikakati mbalimbali inayokwenda sambamba na uhamasishaji wa shughuli za ujasirimali, mwamko huo utaongezeka.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com