Serikali imeahidi kuendelea
kuboresha mifumo ya kukusanya mapato pamoja na kuboresha miundombinu ya
kiuchumi na kijamii ili kuleta unafuu wa maisha ya Wastaafu na Wananchi
kwa ujumla.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mtambile Mhe.
Masoud Abdallah Salim (CUF), aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika
kuboresha mafao ya uzeeni ili kuondoa malalamiko ya hali ngumu ya maisha
wanayoishi Wastaafu.
Mhe. Salim alisema kuwa kumekuwepo
malalamiko mengi kutoka kwa Wastaafu ambao wakati wa utumishi wao
walilitumikia Taifa kwa uwaminifu na uadilifu mkubwa, kuhusu kuishi
maisha magumu yanayotokana na kucheleweshewa mafao yao ya uzeeni
yasiyolingana na kupanda kwa gharama za maisha.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alisema kuwa, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi katika kuboresha
miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma
za afya, elimu na kiuchumi hususan katika ukusanyaji mapato kwa lengo la
kuboresha maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.
“Tuendelee kuiunga mkono Serikali
yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi wa viwanda ambao
ndio msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali”. Alisema Dkt.
Kijaji.
Alisema kuwa maboresho ya viwango
vya pensheni kwa Wastaafu yasiyoendana na maboresho ya miundombinu ya
kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya Wastaafu
hivyo Serikali imelenga zaidi kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii
ili kupunguza malalamiko hayo.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa
nyongeza ya pensheni kwa Wastaafu, mishahara na maslahi mazuri kwa
Watumishi wa Umma itaongezeka kama mikakati na azma ya Serikali ya
kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi itafanikishwa.
Aidha Dkt. Kijaji aliongeza kuwa
Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni ili kukidhi
mahitaji muhimu ya Wastaafu, kwa kutambua hilo Mwezi Julai 2015,
Serikali iliboresha kiwango cha pensheni kutoka Sh. 50,114 hadi Sh.
100,125 kwa mwezi.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
0 comments:
Post a Comment